Twaweza.org

Chanzo cha fikra zetu

Chanzo cha fikra zetu

Katika eneo zima la Afrka Masharika dola zinashindwa kutoa huduma muhimu wanazohitaji wananchi. Mabadiliko ya kisheria yamepiga hatua nzuri, lakini tatizo linajitokeza katika utekelezaji. Viongozi wa serikali na watu wa matabaka ya juu yamejitenga mno na maisha ya wananchi wa kawaida, na hii ni kweli pia hata kwa asasi nyingi zisizo za kiserikali ambazo kazi zake haziratibiwi vyema, zina malengo ya muda mfupi na pia zinategemea sana matakwa ya wafadhili.Vyombo vya habari vimebanwa kutokana na ukiritimba katika miliki na udhibiti juu ya wahariri, na vyombo vya utangazaji vya dola havijaweza kujibadilisha kuwa vyombo vya umma. Katika Afrika Mashariki hakuna mikakati ya muda mrefu inayoweza kuleta mabadiliko makubwa na kukuza utamaduni wa kutenda kwa kutafakari na kujifunza kutokana na uzoefu uliopatikana kuhusu nini kinazaa tija na ni ni hakizai tija. Hata hivyo nafasi ya raia kujifanyai amambo yao wenyewe imekua. Matumizi ya simu za mkononi yameongeza kwa kiasi kikubwa sana fursa za mawasiliano. Vijana ni sehemu muhimu ya jamii zetu na pia ni sehemu muhimu ya kuleta mabadiliko. Kuna ushiriki mkubwa zaidi wa raia katika michakato ya bajeti, ambazo sasa zinachunguzwa na kusailiwa zaidi. Tathmini zetu za nchi hizi ziliibua maeneo sita ambayo yanapewa umuhimu mkubwa katika kazi zetu.

1. Mambo ya kila siku katika ngazi ya chini ndiyo muhimu mno

Ni rahisi kufikiria sera, maboresho na bajeti katika hali ya ujumla wake katika ngazi ya siasa za kitaifa. Lakini ziara zetu katika jumiya zilionyesha msigano mkubwa kati ya ngazi ya kitaifa na kisera na hali halisi ya maisha ya kila siku na jinsi ilivyo rahisi kwa juhudi za mandeleo kushindwa kuiona jamii katika ngazi ya chini. Watu wengi walioulizwa maswali walishindwa kujibu swali lililopangiliwa hivi: “Hii ina maana gani kwa mwanamke wa miaka 45 kijijini? Anaweza kufanya nini?” Lakini ni katika ngazi hii wanakoishi watu, hapa ndipo kuna maisha halisi, na hapa ndipo maisha ya wananchi yanapoathirika—mahusiano na walimu, wafanyakazi wa afya na viongozi wa mitaa, maisha  ya kila siku na fursa za kila siku. Mtazamo wa jumla kuanzia juu ni muhimu kwa jinsi unavyoathiri maisha ya wananchi, lakini kwa sisi Twaweza tunahitaji kuchukua mambo ya kawaida ya kila siku kama mahali pa kuanzia.

2. Upatikanaji wa habari huwawezesha raia kuchukua hatua

Takriban kila tuliyezungumza naye alisisitiza kwamba raia wanahitaji kuhabarishwa ili waweze kuchukua hatua na kuleta mabadiliko. Habari huwawezesha wananchi kujua haki na stahili zao, kujua nini kinatokea karibu yao na mbali pia, kulinganisha kufanya ulinganisho kati ya kilichopo na kilichoahidiwa, kujifunza kutokana na walichofanya wengine, na kadhalika.  Pasipo na habari, ama hakuna hatua zinazochukuliwa ama zitachukuliwa bila weledi wa kutosha.  Funzo moja kubwa ni kwamba, ingawaje habari peke yake haijitoshelezi, lakini ni kichocheo kikubwa na cha lazima katika kuleta mabadiliko.

3. Kuondoa misigano ya kitabaka na kijiografia, na baina ya raia na asasi za kiraia

Watu wenye madaraka na ambao wamekabidhiwa majukumu ya kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida aghalabu huishi na kufikiri wakiwa katika miji mikuu na miongoni mwao wenyewe, wawe serikalini, katika vyombo vya habari katika asasi za kiraia au katika biashara. Tabaka hili la juu halina muunganisho wa kuridhisha baina yake na watu wa chini na hivyo ipo hatari ya kutojua kinachotokea na kudhoofika kwa kukosa kuungwa mkono na jamii pana. Makundi mengi tuliyoyahoji yanatambua kuwapo kwa msigano huu na wameanza kuufanyia kazi, ingawaje kasi imekuwa ndogo na kunahitajika ubunifu zaidi. Kinachohitajika hapa ni kuainisha uhusiano kati ya uhamasishaji (kukusanya idadi kubwa ya watu kuunga mkono hoja) na oganaizesheni (kuwasaidia watu kujipanga kufanya uratibu wa jinsi ya kulisukuma jambo lao).

4. Kuunganisha juhudi zilizosambaa

Katika nchi zote tatu tuliweza kutambua juhudi za kibunifu na zenye manufaa. Lakini juhudi hizi zinafanyika vipande vipande na hivyo zinashindwa kuwa na msukumo mkubwa wa kuleta mabadiliko au kuwa na athari kubwa. Watu wengi tuliozungumza nao wanaona ni vyema kuunganisha watu na mawazo ili kuleta mabadiliko makubwa zaidi, na wamepongeza mtazamo wa mfumo-hali wa Twaweza.

5. Kujifunza, tafakuri na ubunifu ni muhimu

Washiriki wengi katika michakato ya maendeleo hutumia muda wao kukimbia huku na huku wakitafuta fedha, wakiendesha asasi zao, wakitekeleza miradi na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kiasi kwamba hawajipi muda wa kutosha ya kufanya tafakuri juu ya mikakati na tija inayopatika kutokana na uteuzi wa mikakati. Lakini hili ni jambo muhimu sana katika maisha na siha ya mpango wo wote. Kuhusu hili, watu wengi mshuhuri walipendezewa na mwelekeo wa Twaweza toka mwanzo, na pia waliipongeza Twaweza kwa kile ambacho mmoja wao alikiita 'tafakuri nzito'.

6. Mabadiliko ya kina huchukua muda

Watu wengi walisema jambo moja ambalo si gumu kulielewa – mabadiliko ya aina inayotafutwa na Twaweza yatachukua muda. Msemo uliosikika mara nyingi ulikuwa : "Kama huwezi kufikiri kwa kuangalia kipindi cha miaka saba hadi kumi au zaidi ijayo, wala usijisumbue".  Wengine walituasa tujihadhari na wafadhili wanaotaka matunda ya haraka. Badala yake kinachohitajika ni kuwa na mtazamo wa muda mrefu na ubunifu unaoruhusu kutumia kila fursa muhimu. Twaweza pamoja na wabia wafadhili wake haina budi kufanya kazi kwa karibu ili kuweka uwiano mwafaka katika hili.

Endelea kusoma: maadili ya kazi

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri