Twaweza.org

Ndoa za Utotoni Hupunguza Ubora wa Maisha kwa Wasichana wadogo na Watoto wao

Katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani 2020, vijana wawili wanaharakati wa kitanzania wamezindua filamu yao kuhusu ndoa za utotoni kwa kushirikiana na Msichana Initiative na Twaweza. Elias Maeda na Festo Henry Msangawale ni watetezi wa haki za kijinsia ambao wanalenga kufikisha ujumbe kwa jamii na viongozi wote nchini kuchukua hatua kuwasaidia wasichana wa umri mdogo kutimiza ndoto zao kwa kukomesha ndoa za utotoni.

Ingawa sheria inawalinda wasichana wadogo shuleni dhidi ya kuolewa na kukatisha masomo kupitia Sheria ya Elimu, Sheria ya Ndoa inaruhusu wasichana kuolewa wakiwa chini ya umri wa miaka 18. Hii inamaanisha kuwa wasichana walio nje ya mfumo wa shule, tayari wako hatarini zaidi kutolindwa na sheria. Hivi sasa, kuna amri ya Mahakama inayotaka Sheria ya Ndoa pia ibadilishwe ili kuwalinda wasichana wote wa umri mdogo. lakini amri hii bado halijatekelezwa.

Nchini Tanzania, wasichana 2 kati ya 5 wameolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18. Nchi inaweza kuwa inapoteza kiasi cha Tsh milioni 637 kila mwaka (ilikadiriwa, 2015) mapato yanayopotea kwasababu ya ndoa za utotoni. Aidha, takwimu zinaonesha kuwa 1% tu ya wasichana wadogo wenye umri wa miaka 15 hadi 19 ambao wameolewa wapo shuleni, ikilinganishwa na 45% ya wavulana wa umri huo huo ambao hawajaoa. Takwimu zinaonesha zaidi kuwa akina mama wenye elimu wanahakikisha watoto wao wana afya bora kuliko wenzao wasio na elimu.
●    41% ya wanawake wasio na elimu rasmi hujifungua katika vituo vya afya ikilinganishwa na 89% ya wenzao waliosoma kwa kiwango cha sekondari au zaidi
●    Wanawake wasio na elimu rasmi wana uwezekano mdogo (38%) kuliko wale walio na elimu ya sekondari au zaidi (64%) kuwahi kutafuta matibabu kwa mtoto aliye na homa ndani ya siku moja
●    Watoto wa akina mama wasio na elimu rasmi wana uwezekano mkubwa zaidi wa kupimwa na kukutwa na malaria, 21%, kuliko wale ambao mama zao wana elimu ya sekondari au ya juu (4%).

Filamu fupi iliyotengenezwa na wanaharakati vijana, Elias Maeda na Festo Msangawale, inagusa masuala yote ya msingi ya ndoa za utotoni. Katika filamu hiyo, inayoitwa Hellena, wazazi wanasukumwa na shauku yao ya kumwozesha binti yao. Ndoa za utotoni huathiri vibaya familia masikini: wanawake kutoka kaya masikini wana uwezekano mkubwa wa kuolewa wakiwa watoto (46%) ikilinganishwa na wenzao kutoka familia tajiri (16% waliolewa wakiwa bado ni watoto). Wanawake wa vijijini pia wana uwezekano mkubwa kuliko wanawake wa mijini kuolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18 (37% dhidi ya 21%).

Wasichana wakiolewa wakiwa watoto wana fursa ndogo sana ya kupata elimu. Kati ya wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 19 ambao wameolewa, ni 1% tu wapo shuleni ikilinganishwa na 45% ya wasichana wa umri huo ambao hawajaolewa. Na hiki ndicho anakijutia sana Hellena kuhusu hali yake kwenye filamu - anataka kumaliza masomo yake na kuwasaidia wazazi wake siku zijazo.

Vivyo hivyo, 60% ya wanawake ambao waliolewa wakiwa watoto wanafanya kazi kwenye kilimo (wakulima) ukilinganisha na 39% ya wanawake ambao waliolewa wakiwa na umri wa miaka 20 au zaidi. Wanawake ambao wameolewa wakiwa na miaka 20 au zaidi wana uwezekano mkubwa (14%) kuwa na kazi za kitaalam au ujuzi kuliko wenzao walioolewa wakiwa watoto (3%). Kwenye filamu hiyo, tunaona Hellena akijitahidi kutimiza majukumu yake mapya katika kazi ya kilimo ingawa alikuwa na ndoto ya kuwa rubani wa ndege.

Pia wasichana wadogo ambao wameolewa wakiwa watoto wanasumbuliwa sana na masuala ya kisaikolojia. Wanawake ambao wameolewa mapema wana uwezekano mkubwa wa kusema ni sawa kwa mume kumpiga mkewe ikiwa atatoka bila kumwambia (47%) ikilinganishwa na wale ambao waliolewa wakiwa na umri wa miaka 20 au zaidi (37%). Pia wana mamlaka/nguvu ndogo ya kufanya maamuzi katika nyumba zao, hasa juu ya fedha. Aidha, wake wenye umri mdogo (watoto) wana uwezekano mkubwa wa kukumbana na ukatili wa kimwili na kingono kuliko wenzao walioolewa wakiwa na umri mkubwa.

Endelea kusoma:

featured

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri