Twaweza.org

Mimi ni Mwalimu | Kalenda 2014

Twaweza imechapisha kalenda ya mwaka 2014, mkazo ukiwa katika sekta ya elimu. Dhumuni kuu la kalenda hii ni kuwahamasisha walimu kwa  kuwakumbusha umuhimu wa kazi yao na uwezo wao mkubwa katika kuijenga jamii. Twaweza imefanya hivi kwa kurejea ‘nukuu’ kadhaa  na picha za  Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Julius Kambarage Nyerere.  Nyerere alifahamika zaidi kwa jina la ‘Mwalimu’  kwani kwa miaka mingi alikuwa mwalimu na aliipenda sana kazi yake, akiiheshimu na kusisitiza umuhimu wa elimu katika maendeleo na pia jukumu kubwa wanalolibeba walimu.

Kwa kutumia kumbukumbu hii ya mmoja kati ya mashujaa walioheshimiwa sana nchini, ni lengo letu kuhamasisha walimu waendelee kushiriki katika juhudi zao za kuboresha maendeleo ya Watanzania.

Twaweza ilifanikiwa kupata picha za Mwalimu Nyerere, ambazo hazipatikani kirahisi kwa umma kutoka Idara ya Habari Maelezo. (Ambazo hazipo wazi kwa jamii.) Kalenda hii imebeba jumbe zifuatazo:

  • Ualimu ni kulea.
  • Kujifunza hakuna kikomo.
  • Ualimu ni burudani.
  • Ualimu ni unyenyekevu.

Kalenda hizi zimechapishwa kwa ushirikiano na Chama cha Walimu Tanzania na zimesambazwa kwa walimu wote nchini kwa kupitia taasisi hii.

Pamoja na nakala hizi za kalenda, kila mwalimu atapokea kadi itakayomuomba aandike, kwa maneno yake mwenyewe, ahadi ya kuwa ataenzi ujumbe uliondikwa kwenye kalenda hizi. Pia zawadi zitatolewa kwa ahadi mia mbili bora zitakazowasilishwa.

Kupitia kadi hizi, Twaweza itakuwa na uwezo wakuelewa maoni ya walimu kuhusu kazi zao. Hadi sasa, mrejesho wa awali umekuwa wa kufurahisha.

Endelea kusoma: elimu

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri