Twaweza.org

Mpango wa KiuFunza - Kiu ya Kujifunza - Wazinduliwa

Mpango mpya wa utekelezaji wa sera za Elimu, inayojulikana kama KiuFunza, itakayojaribu kutekeleza utaratibu wa kupeleka kiasi kamili cha ruzuku kwa kila mwanafunzi moja kwa moja shuleni kwa ajili ya uendeshaji wa shule; na kuwalipa walimu motisha kwa ufundishaji makini umezinduliwa. Mpango wa KiuFunza unalenga kutafuta njia bora zaidi za kuinua matokeo ya ujifunzaji kwa wanafunzi katika shule za msingi.

Mpango huu utatekelezwa katika Halmashauri 11 zilizochaguliwa kinasibu katika kipindi cha 2013 na 2014. Katika kila Halmashauri shule 35 zitashiriki. Wilaya zitakazohusika katika mpango huu ni: Karagwe, Kigoma Vijijini, Geita, Kahama, Kondoa, Korogwe Vijijini, Lushoto, Sumbawanga Vijijini, Mbozi, Mbinga na Kinondoni.

KiuFunza ni jitihada inayotekelezwa kwa ushirikiano baina ya Twaweza, Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), na watafiti wa kimataifa kutoka Abdul Latif Jameel Poverty Action Lab (J-PAL) ya Massachusetts Institute of Technology (MIT). Lengo la mpango huu ni kupata ushahidi wa kuaminika kisayansi, kupitia utafiti makini, kuhusu mbinu ambazo zina ufanisi wa uhakika katika kuwasaidia wanafunzi kujifunza. Mpango huu utajaribu kutekeleza njia mbadala ya kutekeleza sera ya sasa ya kupeleka ruzuku ya uendeshaji shuleni, na pia utatekeleza mbinu mpya ya kuwalipa walimu motisha ya fedha kwa ufundishaji makini utakaofanya matokeo ya kujifunza kwa wanafunzi kuwa bora kuliko ilivyo sasa.

Mpango huu wa utafiti ulizinduliwa katika semina ya Wadau iliyofanyika katika Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa tarehe 23 Januari, 2013. Mgeni rasmi katika semina hiyo alikuwa Mh. Hawa Ghasia (MB), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Watoa mada walitoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Chama cha Walimu Tanzania (CWT), waheshimiwa wabunge, na Twaweza. Mikoa na halmashauri zitakazoshiriki katika utekelezaji wa mpango huu pia ziliwakilishwa na Makatibu Tawala, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wenyeviti wa Halmashauri na Maafisa Elimu. Wabunge pia walishiriki. 

Endelea kusoma (Kiingereza)

Endelea kusoma: elimu

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri