Twaweza.org

KiuFunzaII: Malipo baada ya matokeo kwa walimu kuboresha matokeo ya kujifunza katika madarasa ya mwanzo

Baada ya miaka miwili ya majaribio, Twaweza, kwa kushirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na shirika la Innovations for Poverty Action (IPA), wamedhihirisha kuwa kuwalipa walimu fedha baada ya matokeo ya kujifunza kunaweza kuboresha matokeo ya kujifunza. Matokeo haya yamethibitisha kwamba wanafunzi wameweza kujifunza na kupata stadi stahiki kwa muda wa mwaka mmoja kile ambacho wangeweza kujifunza kwa mwaka na nusu muhula.

Matokeo ya utafiti unaojulikana kama KiuFunza, utafiti mkubwa wa aina yake Afrika Mashariki, yaliwasilishwa katika majadiliano na wadau wa elimu jijini Dar es Salaam.

Kwa kipindi cha miaka miwili ya KiuFunza, Twaweza na IPA wamefanya majaribio yafuatayo katika shule 200 kwenye wilaya 21 za Tanzania:

 • Kutoa bahshishi kwa kujifunza stadi mahususi zilizoainishwa kwa darasa kwenye kundi moja la shule (Stadi).
 • Kutoa bahshishi kwa ongezeko la kujifunza kwenye kundi lingine la shule (Mashindano).

Njia zote mbili zilijaribiwa ili kulinganisha matokeo yaliyopatikana na kundi la shule zilizohusishwa moja kwa moja. Japokuwa mfumo wa Mashindano ni mgumu zaidi kueleweka kuliko mfumo wa Stadi, mfumo huu huleta usawa zaidi kwa walimu, kwakuwa wanafunzi hushindana na wenzao walio kwenye makundi yenye uwezo unaofanana. Stadi  hueleweka kwa urahisi zaidi lakini pia huwapendelea walimu wanaofundisha wanafunzi wenye uwezo mkubwa (mara nyingi wa shule za mijini).

Wastani wa bahshishi waliyolipwa walimu wa masomo ni shilingi 266,315.00 sawa na karibu asilimia 42 ya wastani wa mshahara wa kila mwezi (kabla ya kodi) mwaka 2016. Kiwango cha chini cha fedha kilicholipwa kilikuwa shilingi 8,100 ambapo ni walimu wachache tu ambao hawakuambulia kitu. Mwalimu aliyelipwa kiasi kikubwa kuliko wote alipata shilingi milioni 3.6.

Mbali na kuboresha matokeo ya kujifunza, mfumo wa kuwalipa walimu bahshishi umeonekana kuungwa mkono na walimu wengi:

 • Walimu tisa kati ya kumi kwenye shule za majaribio wanaunga mkono wazo la malipo kwa matokeo.
 • Walipoulizwa kuhusu utaratibu huu kuwa la kisera, asilimia 63 ya walimu waliafiki kwamba Serikali iweke mfumo rasmi wa motisha kwa walimu kutokana na matokeo mazuri wakati yatakapofanyika maboresho ya mishahara (lakini asilimia 37 walisema kiwango cha malipo hayo kiongezwe na kiwe sawa kwa wote)

Mwaka 2016

 • Kulikuwa na shule 135 kutoka wilaya 21 zilizoshiriki kwenye utafiti na shule 60 zilitumika kwa ajili ya kulinganisha.
 • Jumla ya wanafunzi 65,643 walipimwa wakiwemo wanafunzi wa shule za ulinganisho.
 • Kwa ujumla, wanafunzi 48,042 walikuwa katika shule ambako motisha ilitolewa na hivyo walifanikiwa kujifunza zaidi kuliko wenzao.


Matokeo haya ni kutoka awamu ya pili ya KiuFunza 2015 -2016. Awamu ya kwanza 2013 – 2014 Twaweza ilifanya jaribio la kupeleka fedha za ruzuku moja kwa moja shuleni (utaratibu huu unatumiwa na Serikali kuanzia Januari mwaka 2016) na Malipo kwa walimu ya matokeo ya kujifunza pekee na kwa kuchanganya ruzuku na bahshishi. Awamu hii ya I ilionesha matokeo chanya ya kujifunza pale ambapo motisha kwa walimu na upelekaji wa fedha za ruzuku moja kwa moja shuleni vilipochanganywa. Awamu ya pili ilijaribu mifumo makini zaidi ya utoaji wa motisha baada ya upelekaji wa Ruzuku ya uendeshaji wa shule moja kwa moja shuleni kuanza kutekelezwa na serikali.

Twaweza imechagua kujikita kwenye utoaji wa motisha kwa walimu katika awamu ya kwanza na ya pili ya KiuFunza kwasababu ushahidi kutoka maeneo mbalimbali duniani unaonesha kuwa motisha huwahamasisha walimu kuongeza jitihada na kuleta matokeo chanya ya kujifunza. Kwa kuongezea, KiuFunza (na tafiti nyingine) zinaonesha wazi kuwa motisha kwa mwalimu na uwajibikaji ni mambo ambayo yamekosekana shuleni. Wakati wa ziara za kushtukiza katika shule za msingi mwaka 2016:

 • 41% ya walimu walikuwa darasani wakifundisha.
 • 27% hawakuwepo shuleni.
 • 32% walikuwepo shuleni lakini hawakuwepo darasani kufundisha.
 • Shillingi bilioni 793 zinakadiriwa kupotea kila mwaka kutokana na walimu kutohudhuria darasani.

Endelea kusoma: kujifunza

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri