Twaweza.org

Serikali na wadau wa Elimu nchini tushirikiane kuboresha matokeo ya kujifunza

Makala hii imechapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la Mwananchi na Greyson Mgoi - Afisa Mawasiliano wa Uwezo-Tanzania, Twaweza.

KUTOKUWA na Usawa katika kujifunza maana yake ni kutokuwa na uwiano ulio sawia wa rasilimali na huduma za elimu zinazoathiri matokeo ya kujifunza.  Mfano wa rasilimali hizo ni ruzuku itolewayo kwa kila shule, walimu wenye sifa na wazoefu, idadi ya vitabu, majengo na uwepo wa teknolojia wezeshi katika kujifunza.

Elimu aipatayo mtoto anayesoma shule ya Msingi au sekondari ya umma iliyoko kijijini si sawa na ya yule anayesoma katika darasa hilo hilo kwenye shule ya mjini.

Hivi sasa tumekuwa tukiona matokeo ya mitihani ya kidato cha nne na cha sita hapa nchini, kuwa watoto wanaosoma shule za binafsi ambazo kwa kawaida zina miundombinu mizuri na vifaa vya kujifunzia, wamekuwa wakifanya vizuri kwenye matokeo hayo kuwazidi watoto wanaosoma shule za umma (Rejea matokeo ya kidato cha nne mwaka 2017, shule kumi bora na shule kumi za mwisho)

Utafiti uliofanywa na Uwezo iliyoko Twaweza kwenye ripoti iitwayo “Je, Watoto Wetu Wanajifunza?” unaonesha kwamba Bado hakuna usawa kwenye matokeo ya kujifunza, pia kwenye vifaa na huduma zipatikanazo shuleni.

Utafiti huo unaeleza kuwa, miongoni mwa watoto wenye umri wa miaka 9 hadi 13 nchini, asilimia 38 hawawezi kufanya majaribio ya darasa la 2 huku tofauti kubwa ikionekana katika wilaya. Inafafanua kuwa, ambapo Wilaya ya Iringa Mjini, inayoongoza kwa ufaulu, asilimia 75 ya watoto wenye umri wa miaka 9 hadi 13 wana uwezo wa kufaulu majaribio ya kusoma Kingereza na Kiswahili na kufanya hesabu rahisi, huku Wilaya ya Sikonge ambayo imefanya vibaya, ni asilimia 17 pekee ya watoto walioweza kufaulu majaribio hayo.

Kimkoa, asilimia 64 ya wanafunzi mkoani Dar es Salaam wenye miaka 9 hadi 13 wana uwezo wa kufaulu majaribio yote matatu, lakini kwa upande wa wenzao mkoani Katavi ni asilimia 23 pekee ya watoto wanaoweza kufaulu majaribio hayo. Kwa ujumla tofauti kati ya maeneo ya vijijini (51%) na mijini (65%) haijajitokeza sana kama tofauti iliyopo kwenye maeneo maalumu.

Aidha ripoti ya Uwezo inabainisha kuwa, Mkoani Dar es Salaam, ni asilimia 16 pekee ya wanafunzi wenye umri wa miaka 11 ambao wapo nyuma mwaka mmoja wa masomo ama zaidi. Mkoani Katavi idadi hiyo imeongezeka na kufikia 72%.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa eneo analoishi mtoto lina mchango mkubwa kwenye matokeo ya kujifunza kuliko umasikini na mambo mengine yaliyokuwa yakiainishwa hapo awali. Watoto wanne kati ya kumi (42%) kutoka kaya masikini sana walifaulu majaribio yote matatu ukilinganisha na karibu watoto sita kati ya kumi (58%) kutoka kaya zenye uwezo.

Mkurugenzi wa Twaweza ndugu Aidan Eyakuze akizindua ripoti hiyo alisema kuwa tafiti nyingi zimeonesha ambavyo uwezo wa mali katika kaya unavyoathiri fursa na matokeo ya elimu. Lakini, takwimu hizi zinaonesha kuwa maeneo wanayoishi watoto hasa maeneo ya pembezoni mwa nchi, huchangia kwa kiwango kikubwa namna wanavyojifunza ama kutojifunza. Eneo anakoishi mtoto lina mchango mkubwa zaidi kwenye matokeo ya kujifunza kuliko umasikini, kiwango cha elimu ya mama, au iwapo mtoto amesoma shule ya awali au la.  Japokuwa ipo sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu suala zima la usawa katika kupata huduma ya elimu bora, takwimu hizi zinatoa fursa kwa watunga sera kuelekeza juhudi na rasilimali kwenye maeneo ya pembezoni zaidi na kwa watoto wenye uhitaji zaidi.

Pia taarifa ya Twaweza inafafanua kuwa, matabaka katika kujifunza yanajitokeza kwenye mlolongo wa vizazi; ambapo matokeo ya tafiti yanaeleza kuwa, watoto watatu kati ya wanne (74%) ambao mama zao wana elimu ya sekondari au elimu ya juu, walifaulu majaribio yote matatu ukilinganisha na 46% ya watoto ambao mama zao hawakusoma.

Sambamba na hayo, tafiti hiyo inaeleza kwamba, matabaka kutokana na eneo yana onekana pia katika vifaa, rasilimali na huduma zipatikanazo shuleni. Mfano, Mkoani Dar es Salaam, nusu ya shule (51%) zina huduma ya umeme wakati mkoani Geita, ni shule 2 tu (4%) kati ya 50 zinazopata huduma hiyo. Mkoa wa Geita pia huduma ya maji si ya kuridhisha ambapo ni asilimia 12 tu ya shule zina huduma ya maji safi na salama wakati mkoani Kilimanjaro, karibu shule 8 kati ya 10 (78%) zina huduma hiyo.  

Pia takwimu zinaeleza kuwa, Mkoani Kilimanjaro, wanafunzi 26 wanatumia choo kimoja, lakini mkoani Geita ni wanafunzi 74, au mara tatu zaidi ya wanafunzi. Vile vile asilimia 5 ya shule mkoani Geita zinatoa huduma ya chakula cha mchana wakati mkoani Kilimanjaro ni asilimia 79. Mkoa wa Dar es Salaam, wanafunzi sita wanatumia kitabu kimoja wakati mkoani Kilimanjaro, wanafunzi wawili wanatumia kitabu kimoja, Mkoa wa Kilimanjaro pia ni mkoa unaofanya vizuri kwenye uwiano wa wanafunzi kwa mwalimu (36:1) ukilinganisha na 52:1 mkoani Katavi.

Inabainisha taarifa hiyo kuwa, Utoro wa wanafunzi ni tatizo kote nchini lakini tatizo hili ni kubwa katika baadhi ya maeneo: Mkoani Dodoma asilimia 79 ya wanafunzi walikuwepo siku tathmini ya Uwezo ilipofanyika wakati mkoani Mtwara ni asilimia 61 ya wanafunzi waliokuwepo.

Takwimu za Uwezo zinaonesha wazi kuwa, kukosekana kwa usawa kwenye mfumo wa elimu, kunajidhihirisha katika matokeo ya kujifunza, mgawanyo wa  rasilimali na upatikanaji wa huduma muhimu shuleni kama vile maji safi na salama, chakula na meme. Habari njema ni kwamba sasa tuna mifano hai ya nini kinachopaswa kufanyika ili kurekebisha hali hii hapa nchini.  Serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa watoto na wilaya za mwisho haziachwi nyuma.”  Alinukuliwa Meneja wa Uwezo Tanzania, Zaida Mgalla, akisema.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosaini na kukubalina kutekeleza malengo endelevu ya milenia (SDGs) na miongoni mwa malengo hayo ni lengo namba nne linalohusu utoaji wa elimu bora.

Katika kuhakikisha lengo hili linafanikiwa na watoto wote wanakwenda shule na kupata elimu iliyobora, Rais wa Jamuhuri  ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli mara tu baada ya kuingia madarakani, alitangaza kufuta michango mashuleni,yaani kwenye shule za umma za msingi na sekondari kote nchini , na hapo ndipo utekelezaji wa sera ya Elimu bila malipo ilipoanza kutekelezwa.

Taarifa mbalimbali zinaonesha kuwa Sera ya Elimu bila malipo imefanikiwa kwa kiasi hasa katika kuongezeka kwa idadi ya watoto wanao andikishwa darasa la kwanza. Ingawa bado kuna changamoto ndogondogo zinazo ambatana na utekelezaji wa sera hii. Lakini tunaweza kujivuna na kujigamba kuwa sasa watoto wetu wanasoma bure, hakuna kulipa ada na michango mingine ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa kikwazo kwa watoto wengi kupata Elimu hapa nchini.

Lakini pamoja na elimu kutolewa bure bado kuna changamoto hivyo ni vizuri serikali kwa kushirikiana na wadau wasaidiane kuangalia namna ya kupunguza  au kumaliza kabisa changamto kwa elimu ya watoto wetu ambazo pia zinachangia kuwepo kwa pengo katika kujifunza baina ya wanafunzi wa eneo moja na lingine.

Mdau wa Elimu, Dk Luka Mkonongwa akichangia katika mjadala uliofanyika hivi karibuni wa Uwezo Tanzania kuhusu kukosekana kwa usawa katika kujifunza kwa watoto nchini alisema, “tunahitaji tuwe na msimamo wa kitaifa katika sekta ya Elimu Tanzania, kwa sasa hatuna utaratibu wa kulinda sera ya Elimu, tunayumbishwa na matamko mbalimbali. Kila kiongozi mpya anatoa maelekezo yake kuhusu elimu ya Tanzania na anaweza kubadilisha mfumo wa elimu kadri apendavyo.

“Ni lazima tuwe na utaratibu maalumu wa utoaji wa elimu bora kwa watoto utakaofuatwa na kuheshimiwa na kila mtu” alisema Dk Mkonongwa.

Maoni yangu ni kuwa, kama ambavyo serikali ya awamu ya tano iliamua kutangaza elimu bure na sasa inaitekeleza, sasa kwa kushirikiana na wadau wengine wa Elimu mfano wazazi, watupie jicho na kushughulikia pia changamoto zinazosababisha kuwe na pengo kubwa katika matokeo ya kujifunza miongoni mwa watoto wetu. Hii itafanya watoto wote kupata elimu bora, na pia itapelekea mafanikio mazuri kielimu na kiuchumi kwa wote nchini bila kujali maeneo wanayotoka au familia wanazoishi.Na hatimae wasomi hawa kote nchini walioelimika sawasawa, waliopata elimu bora wote; watatupeleka mapema kwenye nchi ya viwanda kama ilivyo ndoto yetu. Nawasilisha.

Endelea kusoma: Elimu Tanzania

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri