Twaweza.org

Mdahalo wa Uchaguzi Mkikimkiki 2015 wazinduliwa

Twaweza inatangaza uzinduzi wa midahalo iitwayo Mkikimkiki 2015. Midahalo hii imeanzishwa ili kutoa fursa na jukwaa kwa vyama vya siasa kunadi sera zao kwa wananchi. Aidha midahalo hii tawapa wananchi fursa ya kuwahoji na kuwapima wagombea na wataalamu wa vyama vikuu vya siasa.

Mfululizo huu wa midahalo umekuja wakati muafaka. Utafiti ulidhaminiwa na Twaweza, uligundua kuwa wananchi 8 kati ya 10 wanafikiri kuwa wagombea ubunge (78%) na urais (79%) wanapaswa kuwa na midahalo ya pamoja. Mbali na mikutano ya hadhara ya kampeni, wananchi wana nafasi finyu sana ya kuwasikiliza na kuwahoji wagombea na vyama vya siasa kuhusu mitazamo, ilani na sera zao katika nyanja mbalimbali.

Maswali ya wananchi na majibu ya hapo kwa hapo ni fursa muhimu kwa wote kupanua uelewa wa wote kuhusu sera na mipango hiyo..

Wananchi wote wanakaribishwa kuwasilisha maswali yao kupitia mtandao na ujumbe mfupi wa simu (SMS). Vilevile, washiriki wa mdahalo na watazamaji wataweza kuuliza maswali wakati wa midahalo.

Tumeandaa mfululizo wa midahalo minne itakayojikita kujadili ilani za vyama vikuu vitano vya siasa. Midahalo hii itahusu: utaifa; uchumi na kukosekana kwa usawa; huduma za kijamii hususan afya na elimu; na rushwa, utawala bora na uadilifu.

Vyama vitano vya siasa tulivyochagua ndivyo vina wagombea wengi zaidi (ngazi ya ubunge na udiwani) kwenye uchaguzi mkuu ujao. Vimealikwa kutuma wataalam wao kushiriki midahalo itakayojadili maeneo haya muhimu. Wawakilishi hawa watahojiwa na jopo la wataalam wa sekta husika.

Aidha, midahalo mitatu tofauti imepangwa kufanyika kwa ajili ya wagombea nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Urais wa Zanzibar na Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kila mdahalo utachukua masaa mawili na nusu, na utarushwa moja kwa moja na Star TV na Radio Free Africa (RFA),  vyombo vya habari vya mshirika wetu, Sahara Media Group. Midahalo imeandaliwa na Compass Communications na kwenye mitandao ya kijamii itaratibiwa na Jamii Forums.

Ratiba ya midahalo ni kama ifuatavyo:

30 AGOSTI 2015 Utaifa (Mdahalo wa masuala la utaifa kuhoji ilani za vyama)
13 SEPTEMBA 2015 Elimu na Afya (Mdahalo wa masuala la elimu na afya kuhoji ilani za vyama)
20 SEPTEMBA 2015  Mdahalo wa wagombea Urais wa Zanzibar
27 SEPTEMBA 2015 Mdahalo wa wagombea nafasi ya Makamu wa Rais
4 OKTOBA 2015 Uchumi, Ajira na Usawa (Mdahalo wa masuala la uchumi, ajira na usawa kuhoji ilani za vyama)
11 OKTOBA 2015 Rushwa, Uadilifu, Maadili (Mdahalo wa masuala la rushwa na maadili kuhoji ilani za vyama)
18 OKTOBA 2015 Mdahalo wa wagombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Unaweza kuwafuata Mkikimkiki kupitia
Tovuti: www.mkikimkiki.com  Facebook: /Mkikimkiki2015  Twitter: @Mkikimkiki

Fuatilia live kuoitia Star TV, RFA au 

Endelea kusoma: 2015

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri