Twaweza.org

Rais wa watu? Tathmini na matarajio ya wananchi kwa serikali ya awamu ya tano

Uondoaji wa wafanyakazi hewa ulitajwa na asilimia 69 ya wananchi wa Tanzania, kama juhudi mojawapo ya Rais John Pombe Magufuli, wanayoifurahia sana. Elimu bure (asilimia 67) na usimamishwaji wa watumishi wa serikali (asilimia 61) navyo pia vilishika nafasi za juu. Walipoambiwa wataje vitendo ambavyo hawakubaliani navyo, asilimia 32 walitaja kuzuiwa kwa uagizwaji wa sukari na bei elekezi ya sukari. Hatahivyo, asilimia 58 hawapingi kitendo chochote cha Rais. Kwa ujumla kiwango cha kukubalika kwa Rais Magufuli anakubalika na asilimia 96 ya wananchi. Kiwango hiki kinaendana na viwango vya kukubalika kwa marais wa Tanzania waliopita.

Pamoja na hayo, asilimia 88 ya wananchi wana imani kuwa Rais Magufuli ataendelea na kasi aliyoanza nayo, mpaka mwisho wa awamu yake ya uongozi.

Viwango vya kukubalika vya viongozi wengine wa serikali pia vipo juu wananchi wanaonekana kumkubali mwenyekiti wao wa kijiji/mtaa (asilimia 78), diwani wao (asilimia 74) na mbunge wao (asilimia 68).

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye utafiti uitwao Rais wa Watu? Tathmini na matarajio ya wananchi kwa serikali ya awamu ya tano. Muhtasari huu unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, ambao ni utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi. Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,813 kutoka maeneo yote Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya) kati ya tarehe 4 Juni na tarehe 20 Juni 2016. 

Wananchi wengi wanasema serikali ya awamu ya tano imeleta maboresho kwenye huduma nyingi za umma. Inayoongoza ni Mamlaka ya Mapato Tanzania ambapo asilimia 85 ya wananchi wanasema huduma zimeboreshwa chini ya serikali mpya. Wananchi pia wanasema huduma ni nzuri mashuleni (asilimia 75), vituo vya polisi (asilimia 74), mahakamani (asilimia 73), vituo vya afya (asilimia 72) na mamlaka za maji (asilimia 67). Ni vema ikafahamika kuwa takwimu hizi zinaonyesha mitazamo na maoni ya wananchi kuhusu huduma za umma na siyo lazima ikawa ndiyo hali halisi ya mabadiliko kwenye huduma hizo. Vilevile, karibu wananchi wote (asilimia 95) wanasema watumishi wa umma wanaotoa huduma, kama madaktari, walimu, pamoja na maofisa tawala wa umma wamekuwa wakiwajibika zaidi. 

 

Endelea kusoma:

Authors: John Mugo

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri