Twaweza.org

Dawa zipo au zimekwisha?

Je, unafahamu kuwa wagonjwa wawili kati ya watano (41%) wanaripoti kutokufanikiwa kupata dawa walizoandikiwa katika vituo vya afya vya umma? Wakati huo huo, familia mbili kati ya tatu nchini Tanzania zinaripoti kuwa walau mwanakaya mmoja aliugua katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita. Hivyo basi, upatikanaji wa dawa unaonekana kuwa ni suala linalogusa maisha ya mamilioni ya wananchi.

Maswali yafuatayo yanaibuka; Ni wapi wananchi wanapata matibabu? Ni kwa namna gani wanapata dawa wanazozihitaji? Je, watumishi wa afya wanamchango gani katika kuzuia au kuhamasisha utoaji wa dawa kwa wagonjwa? Utafiti wa Sauti za Wananchi, ambao ni utafiti kwa njia ya simu za mkononi uliowakilisha Tanzania Bara ulijitahidi kuchunguza.

Maswali haya yalijibiwa na shirika huru la Twaweza katika muhtasari wa utafiti uitwao Dawa zipo au zimeisha? Upatikanaji wa dawa Tanzania.  Matokeo yalionekana kutoa habari njema kuhusu chanjo, chanjo zikiwa ni sehemu muhimu katika huduma ya kinga ya afya. Karibu vituo vyote (96%) vya afya viliripoti kutoa chanjo, asilimia 80% ya vituo hivyo vikiwa pia na akiba ya kutosha ya chanjo hizi. Zaidi ya hayo, nusu ya wagonjwa wote waliotembelea vituo vya afya na kukutwa na malaria, waligundua kuwa idadi kubwa (90%) ya vituo hivi vilikuwa na akiba nzuri ya dawa ya kutibu malaria (Alu).

Lakini siyo taarifa zote zilizotoa matokeo mema. Utafiti wa viashiria vya Utoaji Huduma ya mwaka 2010 ulionyesha kuwa robo (24%) ya dawa muhimu, kwa wastani, hazikuwepo kwenye vituo vya afya nchini kote. Vivyo hivyo, dawa aina ya Alu, ambayo ilitolewa kwa punguzo kupitia mpango wa Serikali na wahisani, mara nyingi ilikuwa ikiuzwa kwa bei ya juu zaidi kuliko hiyo iliyokuwa imeteuliwa. Ni vituo vya afya asilimia 37 tu, na maduka ya dawa asilimia 29 tu yaliyokutwa yakiuza dawa hii kwa bei iliyopendekezwa na serikali.

Endelea kusoma: afya

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri