Twaweza.org

Mwanga Mpya? Maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko kwenye sekta ya elimu

Asilimia 88 ya wananchi wote wanaamini kuwa ahadi ya elimu bure itatekelezwa katika muda uliopangwa; hii ikionesha dhahiri kuwa wananchi wana imani na ahadi hiyo.  Asilimia 76 wanaamini kuwa elimu bure itakuwa elimu bora zaidi. Lakini pamoja na wananchi wengi kuwa na mtizamo chanya, asilimia 15 wanaamini elimu ya bure haitaboresha elimu. Hii ni kutokana na ongezeko kubwa la uandikishwaji wa wanafunzi ambao utatumia rasilimali nyingi.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la Mwanga Mpya? Maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko kwenye sekta ya elimu. Muhtasari huu umetokana na takwimu za Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika mara kwa mara kwa njia ya simu za mkononi. Takwimu zilizokusanywa kati ya tarehe 10 Desemba, 2015 na tarehe 2 Januari 2016, kutoka kwa wahojiwa 1,894 wa Tanzania Bara (Zanzibar haimo kwenye matokeo haya).

Utoaji wa elimu bure pamoja na kukomesha michango shuleni kulikuja katika wakati muafaka. Wazazi wengi walikuwa wanaelemewa na michango ya shule. Kwa ujumla, asilimia 89 ya wazazi wanakiri kulipa michango shuleni; asilimia 80 wakiripoti kulipa mpaka TZS 50,000 kwa mwaka, huku asilimia 8 wakilipa zaidi ya TZS 100,000 kwa mwaka. Asilimia 49 wanaamini kwamba michango yao haitumiki ipasavyo na asilimia 58 wanasema michango hiyo haijaidhinishwa na serikali. Asilimia 89 wanasema walimu hutumia michango hii kujiongezea kipato.

Kwa mujibu wa wazazi, michango hutumika kulipia ulinzi (asilimia 66), majaribio (asilimia 57) na madawati (asilimia 34), huku kiwango kidogo kikielekezwa kwenye mahafali (asilimia 4), pamoja na safari za kishule (asilimia 4). Ruzuku inayopelekwa moja kwa moja shuleni ambayo ndiyo chanzo kikuu cha fedha kwa shule, inaweza isitoshe kuziba pengo la michango iliyoondolewa. Ruzuku inayotolewa huelekezwa kwenye vitabu na nyenzo nyingine za kujifunzia (asilimia 40), vifaa vya kuandikia (asilimia 20), utawala (asilimia 10), pamoja na karatasi za mitihani na uchapaji (asilimia 10).

Hivyo basi, shule zinapaswa kuwa makini na kiwango kidogo cha fedha kinachopatikana, kwani vitu vingi ambavyo wazazi huchangia havijajumuishwa kwenye ruzuku.

Pamoja na wananchi kuwa na imani na ahadi ya elimu bure, wengi wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya ubora wa elimu ya msingi kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita. Asilimia 49 ya wananchi wanasema ubora wa elimu umeongezeka, lakini asilimia 36 wanasema elimu imezorota na asilimia 14 wanasema hakuna mabadiliko yoyote.
 

Endelea kusoma:

Authors: Sana Jaffer

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri