Twaweza.org

Hima tujenge nyumba moja! Watanzania wana maoni gani kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki

Wananchi wanane kati ya kumi (80%) wanafikiri kuwa Tanzania inapaswa kubakia ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Aidha, wananchi tisa kati ya kumi (85%) wanakubali uwepo wa ushirikiano mkubwa zaidi na Kenya na Uganda. Wananchi sita kati ya kumi pia wanauunga mkono upanuzi wa ushirikiano na Rwanda (62%) pamoja na Burundi (59%).

Matokeo haya yalitolewa na Twaweza ikishirikiana na Society for International Development (SID) katika utafiti wenye jina la Hima tujenge nyumba moja! Watanzania wana maoni gani kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki. Msingi wa muhtasari huu ni takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza wenye uwakilishi wa kitaifa barani Afrika unaofanywa kwa kutumia simu za mkononi uliohoji washiriki kutoka kaya mbali mbali Tanzania Bara. Takwimu zilikusanywa Agosti 2014.

Mbali na kuunga mkono ushirikiano huu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wananchi kwa ujumla wanaamini athari zake zitakuwa chanya. Kipengele kilichoaminika kuliko vyote ni kile cha uchumi; wananchi mara mbili kwa wingi wanafikiri kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki itakuwa na athari chanya kiuchumi (42%), ikilinganishwa na wanaofikiri italeta athari hasi (20%). Vile vile, wananchi wengi wanafikiri Jumuiya ya Afrika Mashariki itakuwa na athari chanya badala ya hasi katika usalama (37% dhidi ya 20%), siasa (35% dhidi ya 25%) na utamaduni (33% dhidi ya 24%).

Ingawa wananchi wanaonekana kwa kiasi kikubwa kuipendelea Jumuiya ya Afrika Mashariki na ushirikiano mkubwa zaidi kwa ngazi ya dhana; matokeo ya kuvutia zaidi yalijitokeza walipoulizwa kutoa mapendekezo mahususi. Msimamo wao ulikuwa dhahiri. Zaidi ya nusu ya wananchi wanakubali mapendekezo yafuatayo:

  • Visa ya pekee ya utalii kwa kanda (82% wamekubali)
  • Uwezo wa kusafiri katika kanda kwa kitambulisho cha taifa (82% wamekubali)
  • Miradi ya pamoja ya miundombinu (78% wamekubali)
  • Uhuru wa raia kufanya kazi popote ndani ya nchi wanachama (69% wamekubali)
  • Pasi ya kusafiria moja (67% wamekubali)
  • Biashara huru (bila kodi) (58% wamekubali)
  • Sarafu moja (55% wamekubali)

Mapendekezo pekee ambayo hayakukubaliwa kwa wingi (kishindo) ni kuundwa kwa jeshi la pamoja (64% wamekataa), uhuru wa kumiliki ardhi (70% wamekataa) na Serikali moja yenye Bunge moja la Jumuiya ya Afrika Mashariki (71% wamekataa).

Endelea kusoma:

Authors: Angela Ambroz

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri