Twaweza.org

Kuelekea Kura ya Maoni: Maoni ya Watanzania kuhusu Katiba Inayopendekezwa

Wakati kura ya maoni inakaribia, wananchi wamejigawa katikati. Zaidi ya nusu yao (asilimia 52) wanasema wataunga mkono Katiba Inayopendekezwa. Lakini mwananchi mmoja kati ya wanne (asilimia 26), sawa na nusu ya wanao tayarajia kuiunga mkono katiba, wanasema wataipinga. Mwananchi mmoja kati ya watano (asilimia 22) bado hajamua.

Mnamo mwaka 2014, wakati rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba (CRC) inajadiliwa, wananchi wengi (asilimia 65) walisema wangepiga kura kuikubali rasimu hiyo, na wananchi wachache (asilimia 21) walisema wangeipinga. Ingawa takwimu zinaonyesha kuwa Katiba Inayopendekezwa ingepitishwa na wananchi wa Tanzania Bara, tofauti kati ya makundi haya imezidi kuwa finyu.

Maoni ya wananchi yanaonyesha wazi mashaka yaliyopo katika mchakato mzima wa kuibadili katiba. Mwezi mmoja tu kabla ya siku ya kupiga kura, uandikishaji wa wapiga kura bado haujakamilika. Nusu ya wananchi (asilimia 47) wanafikiri kuwa uchaguzi mkuu ujao utafanyika chini ya katiba mpya, lakini idadi ndogo (asilimia 30) inafikiri kuwa uchaguzi huo utafanyika chini ya katiba ya sasa.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza katika muhtasari wenye jina la: Kuelekea Kura ya Maoni: Maoni ya Watanzania kuhusu Katiba Inayopendekezwa. Muhtasari huu umetokana na takwimu za Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu za mkononi (www.twaweza.org/sauti). Muhtasari huu unajumuisha maoni ya wananchi wa Tanzania Bara (Zanzibar haikuhusishwa katika utafiti huu) juu ya Katiba Inayopendekezwa. Takwimu hizi zinatokana na duru la 29 ya Sauti za Wananchi. Jumla ya wahojiwa 1,399 walipigiwa simu kati ya Januari 27 na Februari 17, 2015. Matokeo mengine yanatokana na duru la 5 la Sauti za Wananchi, (iliyowahoji watu 1,708 kati ya Julai 16 na Julai 30, 2013) na duru la 14 la Sauti za Wananchi (iliyowahoji watu 1,550 kati ya Februari 12 na Machi 4, 2014). Takwimu hizi zimetumika kufuatilia mwenendo wa muda mrefu. Ni muhimu kukumbuka kuwa mahojiano haya yalihusisha makundi yote ya wananchi wa Tanzania Bara.
 

Endelea kusoma:

Authors: Angela Ambroz

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri