Twaweza.org

Demokrasia, udikteta na maandamano: Wananchi wanasemaje?

Demokrasia na uhuru wa kutoa maoni ni vitu viwili vinavyothaminiwa sana na wananchi. Asilimia 95 ya wananchi wanauthamini uwezo wa kuikosoa serikali pale wanapoona imekosea. Na asilimia 69 wanakubali kuwa demokrasia ni mfumo bora wa utawala japokuwa baadhi ya wananchi wanasema kwa kiwango fulani, utawala usio wa kidemokrasia unaweza kukubalika. Hata hivyo asilimia kubwa ya wananchi (asilimia 86) wanasema kuwa Tanzania inahitaji vyama vingi vya siasa ili kuwapa wananchi fursa ya kumchagua kiongozi anayewafaa kuwaongoza.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye muhtasari wake uitwao Demokrasia, udikteta na maandamano: Wananchi wanasemaje? Muhtasari huu unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi. Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,602 kati ya tarehe 23 na 29 Agosti mwaka 2016. Utafiti huu unahusisha Tanzania bara tu. (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya)

Pamoja na kukubalika kwa serikali ya kidemokrasia, wananchi wana maoni tofauti tofauti kuhusu majukumu ya vyama vya upinzani. Asilimia 80 wanasema baada ya uchaguzi, vyama vya upinzani vikubali kushindwa na visaidiane na serikali kuijenga nchi. Ni asilimia 20 tu wanaosema wapinzani waifuatilie na kuiwajibisha serikali iliyopo madarakani. Vilevile, asilimia 49 wanasema mikutano baada ya kipindi cha kampeni hukwamisha maendeleo lakini asilimia 47 wanasema vyama vya upinzani viruhusiwe kufanya mikutano yao bila pingamizi. Huu tena ni mgawanyiko miongoni mwa wafuasi wa vyama: asilimia 71 ya wale wanaoshikamana na vyama vya upinzani wanaunga mkono kufanyika kwa mikutano ukilinganisha na asilimia 37 ya wafuasi wa chama tawala.

Pamoja na hayo, asilimia 60 ya wananchi wanakubaliana na kuzuiwa kwa mikutano ya vyama vya siasa ikihusisha asilimia 70 ya wafuasi wa chama tawala na asilimia 33 ya wafuasi wa vyama vya upinzani. Kwa upande wa ushiriki kwenye maandamano, asilimia 50 hawapo tayari, japokuwa asilimia 29 wapo tayari kuandamana. Wananchi wanaoshikamana na vyama vya upinzani wapo tayari zaidi kushiriki kwenye maandamano (43 asilimia ukilinganisha na asilimia 27 ya wafuasi wa chama tawala) na vijana wanaonekana kuwa tayari zaidi kushiriki kwenye maandamano (asilimia 35 ya vijana wenye umri wa miaka 18-29, tofauti na asilimia 15 ya wananchi wenye umri wa miaka zaidi ya 50).
 

Endelea kusoma: demokrasia

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri