Twaweza.org

Fedha, fedha, fedha! Wananchi na huduma rasmi za kifedha.

Mwananchi mmoja kati ya watano yaani asilimia 22; ana akaunti benki yake mwenyewe au ya ushirika na mtu mwingine. Hili ni ongezeko la asilimia 19 kutoka ilivyokuwa mwaka 2014. Umiliki wa akaunti za benki unatofautiana katika ya makundi mbalimbali: kaya tajiri asilimia 56; kaya masikini asilimia 6; wananchi wa mjini asilimia 41; wananchi wa vijijini asilimia 13; wanaume asilimia 24, na wanawake asilimia 20.

Miongoni mwa wale wasio na akaunti benki (asilimia 78), nane kati ya kumi wanataja kutokuwa na fedha kama sababu kuu ya kutokuwa na akaunti benki.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kupitia muhtasari wake uitwao Fedha, fedha, fedha! Wananchi na huduma rasmi za kifedha. Muhtasari huo unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi. Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,800 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya) kati ya tarehe 14 na 26 septemba 2016.

Idadi ya watu wazima wanaotumia huduma za kifedha kupitia simu za mkononi imeongezeka kutoka asilimia 61 mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2016. Hii inamaanisha kwamba lengo la Serikari la kufikisha huduma za kifedha kwa asilimia 50 ya watanzania ifikapo mwaka 2016 limepitwa kwa kiasi kikubwa. Hii imepelekea serikari kujiwekea Lengo jipya la kufikia asilimia 80 ifikapo mwaka 2017. Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania idadi ya watanzania waliokuwa wamefikiwa na huduma na kifedha kupitia simu za mkononi ilikuwa asilimia 50 mwaka 2014 hivyo basi utafiti huu wa Sauti za Wananchi umeonesha kwamba kuongezeka kwa idadi ya waliofikiwa na huduma hizi ni dalili njema.
Hata hivyo ifahamike kuwa wahojiwa wa Sauti za Wananchi hupewa simu za mkononi ili kufanikisha zoezi la kupata takwimu sahihi zisizo na ubaguzi.

Asilimia 79 ya watumiaji wa huduma za fedha kupitia mitandao ya simu wanasema wanaridhishwa na huduma zinazotolewa. Ni mtumiaji mmoja tu kati ya kumi (asilimia 10) anayesema haridhishwi na huduma hizo. Karibu wote waliosema hawaridhishwi na huduma, wametaja gharama kubwa kama sababu kuu ya kutokuridhishwa kwao. Wananchi  walipoulizwa kuhusu suala la gharama za huduma za fedha kwenye mitandao ya simu za mikononi kwa ujumla, 4 kati ya 10 (asilimia 38) walisema gharama hizo ni kubwa mno.

Endelea kusoma:

Editors: Aidan Eyakuze

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri