Twaweza.org

Kodi ya SIM

Mnamo tarehe 25 Juni, 2013, bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2013/2014 ilipitishwa Bungeni.

Siku chache baada ya kupitishwa kwa bajeti, ilionekana kuwa Serikali ilikuwa imeanzisha tozo ya kila mwezi ya TZS 1,000 kwa kila kadi ya simu ya mkononi (Sim card). Jambo la kushangaza lilikuwa, wabunge pamoja na wananchi wa kawaida waliokuwa wakifuatilia hotuba ya bajeti walidai kuwa kodi hiyo, iliyojulikana kama “Kodi ya Kadi ya SIM”, haikujadiliwa Bungeni. Hili lilizua mjadala wa kitaifa miongoni mwa wabunge wenyewe, makampuni ya simu, vyombo vya habari, wataalamu na wananchi kwa ujumla.

Muhtasari huu unatoa matokeo mapya kuhusiana na mdahalo wa Kodi ya SIM yanatokana na awamu ya tano ya utafiti wa Sauti za Wananchi, ambao ni utafiti wa kwanza wa kitaifa barani Afrika unaokusanya takwimu kwa njia ya simu za mkononi.

Matokeo muhimu ya utafiti huu yalikuwa:

Watanzania walio wengi wana fursa ya kutumia simu za mkononi
Ingawa umiliki wa simu za mkononi uko kwa wingi zaidi katika maeneo ya mijini na hasa kwenye kaya tajiri zaidi, robo tatu ya wakazi wa vijijini walionekana wakiishi katika kaya ambazo walau mwanakaya mmoja alikuwa anamiliki simu ya mkononi. Zaidi ya nusu (52%) ya kaya maskini zilionekana kuwa na walau simu moja.

Kiasi cha tozo cha kodi ni sawa na matumizi ya muda wa hewani ya wiki moja katika kaya maskini
Kwa mujibu wa utafiti huu, kwa wastani, kaya maskini zilionekana zaidi kutumia TZS 3,154 kwa mwezi kwa ajili ya matumizi ya muda wa hewani.  Hii ina maana kuwa walikuwa wanatumia chini ya kiasi cha tozo ya Kodi ya SIM ya TZS 1,000 kwa wiki. Tofauti na kaya maskini, asilimia 10 za kaya tajiri zilionekana kutumia kwa wastani kiasi cha TZS 45,236 kununua muda wa hewani kila mwezi.

Chini ya nusu ya Watanzania wanafahamu kuhusu Kodi ya SIM
Kitaifa, asilimia 46 tu ya wananchi walioonekana kujua kuhusu Kodi ya SIM. Mijini, watu wengi zaidi (55%) walijua kuhusu kodi hiyo. Uelewa wa wananchi wa vijijini kuhusu kodi hii ilikuwa 41% tu.

Watu wengi hawaikubali Kodi ya SIM
Idadi kubwa zaidi, ya 83% katika makundi yote ya vipato, ilionyesha kutokukubaliana na Kodi ya SIM. Miongoni mwa kaya maskini zaidi 71% haikukubaliana na kodi hii. Upinzani mkali zaidi ulitoka kwenye kaya zilizokuwa na kipato bora zaidi, ambapo 86% ya wananchi wanaipinga kodi hiyo.

Endelea kusoma:

Authors: Elvis Mushi

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri