Twaweza.org

Je, Tuko Salama?

Karibu nusu (46%) ya Watanzania wote wamearifu kuwa wameshawahi kushuhudia vurugu katika jamii katika kipindi cha miezi sita iliyopita, ikilinganishwa na idadi ya mtu 1 kati ya 5 (20%) anayeripoti kuwa amewahi kuibiwa kitu na wezi. Nusu (49%) ya Watanzania wote wanaripoti kuwa hawajawahi kuibiwa kitu na watu 4 kati ya 10 (37%) hawajawahi kushuhudia vurugu/ghasia katika jamii.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza katika muhtasari wa utafiti wenye jina la Je, Tuko Salama? Wananchi watoa taarifa kuhusu hali ya usalama wa nchi. Muhtasari huu ni kwa mujibu wa takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti kwa njia ya simu za mkononi wenye uwakilishi wa kitaifa uliofanyika kwenye kaya zote Tanzania Bara.

Wananchi wameripoti kuwa, kesi nyingi walizoshawahi kusikia zinazohusu mtu kutishiwa, kupigwa mawe au kuuawa, huwa ni makundi ya watu au watu binafsi wanaoyatenda na siyo polisi au jeshi. Kwa mfano, mwananchi 1 kati ya 5 (19%) ameshawahi kusikia habari za mtu kuuawa na kundi la watu, wakati ni wananchi 2 kati ya 50 (4%) tu walioshawahi kusikia mtu kuuawa na polisi. Hata hivyo, wananchi pia wamesema kuwa polisi mara nyingi huhusika anapokutwa mtu ametishwa, kupigwa au kupondwa mawe.

Wananchi wanapokumbana na uhalifu, wangependa kuripoti polisi, ingawa, ni nusu tu ya wananchi wote (47%) wanaofanya hivyo. Idadi ni kubwa katika maeneo ya mijini ambako watu 6 kati ya 10 (59%) waliripoti kuwa wangeweza kuripoti uhalifu polisi, ikilinganishwa na maeneo ya vijijini ambako watu 4 kati ya 10 (39%) ndiyo wangefanya hivyo. Hii inaweza kusababishwa na uwepo wa polisi kwenye maeneo ya mijini kuliko vijijini. Kitaifa, kwa mujibu wa maafisa watendaji wa vijiji na wenyekiti wa mitaa/vitongoji, jamii 6 kati ya 10 (62%) haina polisi. Maeneo ya mijini yana nafuu zaidi ambapo mitaa 4 kati ya 10 (36%) tu ndiyo yenye ukosefu wa polisi, wakati maeneo ya vijijini takriban vijiji 8 kati ya 10 (76%) waliripoti kutokuwa na maofisa wa polisi.
 

Endelea kusoma:

Authors: Elvis Mushi

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri