Twaweza.org

Maoni kuhusu Marekebisho ya Sheria ya Takwimu

UCHAMBUZI HUU UMEZINGATIA RASIMU YA AWALI ILIYOTUMWA KWA WADAU. RASIMU YA MWISHO YA MUSWADA ILIFANYIWA MAREKEBISHO YA NYONGEZA YANAYOIPA SHERIA MAMLAKA JUU YA TAKWIMU HURU NA IMESHASAINIWA NA RAIS TANGU TAREHE 24 SEPTEMBA 2018. TUTAWASILISHA HAPA UCHAMBUZI ENDELEVU HIVI KARIBUNI.

Kama mdau muhimu katika tafiti huru na ukusanyaji wa takwimu, Twaweza iliwasilisha uchambuzi wa marekebisho yanayopendekezwa ya Sheria ya Takwimu (2015) kwa kamati husika ya bunge mnamo Agosti 24. Bado hatujaona toleo la mwisho la marekebisho ya sheria hiyo ambalo linadaiwa kuwa limeshawekwa kwenye tovuti ya bunge. Ni vema ikafahamika kwamba, vipengele vya sheria vinavyofanyiwa marekebisho viko huru kupokea mawazo kinzani, kutegemeana na mtazamo wa mtu. Tukiwa kama mdau aneuguswa moja kwa moja na Sheria hii, tungependa kuwasilisha mtazamo wetu kama ifuatavyo:

Kuna mabadiliko kadhaa chanya yaliyofanywa kwenye marekebisho hayo ikiwemo:

  • Kuondolewa kosa la kuchapisha takwimu ambazo ni za “uongo” au “zinazoweza kupotosha ukweli.”
  • Ufafanuzi wa kutosha umetolewa kuhusu tofauti kati ya takwimu rasmi na takwimu zisizo rasmi.
  • Kupunguza baadhi ya makosa yanayohusiana na matumizi mabaya ya cheo/kutotekeleza majukumu ya ajira, n.k na kubakia kwa watumishi wa NBS tu.


Hata hivyo, kuna maeneo mawili yanayotia mashaka. Yote yanahusiana na matakwa ya sheria hii. Sheria hii ina lengo la kusimamia ukusanyaji, uzalishaji na usambazaji wa takwimu rasmi. Takwimu rasmi, kama ilivyotafsiriwa kwenye Sheria na marekebisho yake, ni takwimu zinazokusanywa na taasisi za serikali na NBS au na taasisi zilizopewa mamlaka na NBS ya kukusanya takwimu rasmi. Hata hivyo, marekebisho haya ya 2018 bado yanaendelea kutaja taarifa za takwimu katika namna inayoleta utata. Kwa ufupi ni kama ifuatavyo:

  • Mipaka isiyoeleweka ya mamlaka ya NBS katika kutengeneza kanuni za kukusanya taarifa za takwimu kwa ujumla (nje ya takwimu rasmi). Kifungu 17 (3) (c) kinaitaka NBS “kutunga kanuni kwa ajili ya kukusanya, kuchambua na kuchapisha takwimu kwa ajili ya kuhakikisha taarifa za takwimu zinakuwa na ubora unaoendana, zinapatikana na zinaaminika.”
  • Kuzuia uhakiki wa takwimu rasmi: haijalishi iwapo takwimu rasmi ni za kweli ama la, kwa sasa ni kosa kufanya kwa makusudi uhakiki wa takwimu rasmi na kisha kutoa matokeo hayo hadharani, kwa mujibu wa Kifungu 24 A (2), “Mtu hataruhusiwa kusambaza au kutoa taarifa kwa umma zenye lengo la kukosoa, kupotosha, au kuonesha takwimu rasmi hazifai.”
  • Adhabu zimehusisha taarifa za takwimu wakati kiuhalisia makosa yote yanahusiana na takwimu rasmi. Kifungu 37(4) Mtu yeyote ambaye atachapisha au atakayesababisha kuchapishwa au kutoa taarifa yoyote rasmi ya takwimu au taarifa ya takwimu kinyume cha Sheria hii, atakuwa ametenda kosa.


Tumeona kuwa marekebisho haya mapya ya mwaka 2018, kwa namna yoyote ile, hayazuii ukusanyaji au utoaji wa taarifa za takwimu huru (zinazojulikana pia kama taarifa za takwimu au takwimu zisizo rasmi) kwa namna yoyote:

  • Kwanza, tofauti imeoneshwa kati ya takwimu rasmi na taarifa za takwimu. Marekebisho ya Sheria hii yametoa tafsiri ya maana ya taarifa za takwimu kama ifuatavyo: “taarifa za takwimu zina maana ya taarifa za aina yoyote zinazokusanywa kutoka kwenye vyanzo mbalimbali kupitia sensa, tafiti, au takwimu za kiutawala.”
  • Pili, takwimu rasmi pekee ndizo zinazohitaji kibali cha NBS kabla ya kuchapishwa. Hiki ni kipengele 24A (1): “mtu yeyote ambaye ameruhusiwa na NBS kuchakata takwimu rasmi anapaswa, kabla ya kuchapisha ama kutoa takwimu hizo kwa umma, kupata ruhusa kutoka NBS.” Ni vema ikafahamika kwamba hiki si kipengele kipya na kilikuwemo kwenye toleo la awali la Sheria ya Takwimu.
  • Mwisho, vifungu vyote vinavyogusia mchakato au taratibu za kukusanya takwimu vinatumia dhana ya “takwimu rasmi.” Hizi zimetafsiriwa upya kwenye marekebisho ya Sheria ya Takwimu kama ifuatavyo: “takwimu rasmi” zina maana ya takwimu zinazozalishwa, kupitishwa, kuwekwa pamoja au kusambazwa na, au chini ya mamlaka ya NBS.


Hivyo tafiti zinazofanywa na taasisi kama Twaweza zinaangukia kwenye maana ya “taarifa za takwimu” badala ya “takwimu rasmi” katika toleo la awali la sheria na marekebisho yake.

Nyongeza ya mapitio: Uchambuzi wa Twaweza wa marekebisho yaliyopendekezwa kwenye Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015; kauli kutoka NBS mwaka 2015; kauli ya NBS mwaka 2015 ikifafanua matumizi na mamlaka ya Sheria ya Takwimu (2015).
 

Endelea kusoma:

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri