Twaweza.org

Zege imelala? Maoni ya Watanzania kuhusu kukwama kwa mchakato wa marekebisho ya katiba

Asilimia 67 ya Watanzania wanasema ni muhimu kwa Tanzania kupata katiba mpya na asilimia 56 wanasema toleo la mwisho la rasimu ya katiba lipigiwe kura na wananchi. Hata hivyo, asilimia 48 ya wananchi wanasema kwa maoni yao, katiba mpya haitapatikana ndani ya miaka mitatu ijayo.

Vile vile wananchi wanaendelea kuunga mkono kwa nguvu kubwa uundwaji wa katiba mpya inayotilia mkazo suala la uwajibikaji. Asilimia 79 wanataka mawaziri wanaoteuliwa wapitishwe na bunge na asilimia 64 wanataka wawe na uwezo wa kuwaondoa wabunge katikati ya chaguzi iwapo hawatatekeleza majukumu yao ipasavyo.

Hata hivyo, wananchi wamegawanyika kwenye baadhi ya hatua za uwajibikaji zilizopendekezwa ikiwemo kuzuia viongozi na watumishi wa umma kuwa na akaunti nje ya nchi (asilimia 52 wanaunga mkono), kuwepo kwa ukomo wa ubunge (asilimia 52 wanaunga mkono) na kuweka kanuni za uwazi na uwajibikaji kuwa sehemu ya tunu za taifa (asilimia 48 wanaunga mkono). Hivi vyote ni vipengele vya rasimu ya katiba ambavyo viliondolewa na Bunge Maalumu la Katiba. Pia, wananchi wanaunga mkono kuondolewa kwa kipengele kinachotaka kuchunguza na kudhibiti ofisi ya Rais (asilimia 55) pamoja na mawaziri kuchaguliwa kutoka nje ya Bunge (asilimia 62).

Matokeo haya yametolewa na Twaweza katika utafiti wake uitwao Zege imelala? Maoni ya wananchi kuhusu kukwama kwa mchakato wa kuunda katiba mpya. Muhtasari huu unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi. Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,745 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye utafiti huu) mwezi Juni hadi Julai 2017.

Muundo wa serikali ni moja kati ya vipengele vilivyoibua mjadala mzito wakati wa mchakato wa kuunda katiba mpya na hatimaye kuwagawa wananchi. Asilimia 42 ya wananchi wa Tanzania Bara waliunga mkono muundo wa serikali mbili. Muundo wa serikali moja ulikubalika kwa asilimia 25 tu na muundo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ulipendwa na asilimia 16 tu. Muundo unaoendana na muundo uliopo hivi sasa lakini unaotoa uhuru zaidi kwa Zanzibar uliungwa mkono na asilimia 12. Kukubalika kwa muundo wa serikali unaotumika hivi sasa umeongezeka kutoka asilimia 25 mwaka 2014, hadi asilimia 42 mwaka 2017 na kukubalika kwa serikali tatu kumeshuka kidogo, kutoka asilimia 22 hadi asilimia 16 katika kipindi hicho hicho.

Wananchi wa Zanzibar wana mtazamo tofauti kabisa kuhusu suala hili. Mwaka 2014, asilimia 46 waliunga mkono muundo wa serikali tatu na asilimia 45 waliunga mkono muundo wa serikali mbili uliopo hivi sasa lakini uwe unatoa uhuru zaidi kwa Zanzibar.

Pamoja na maoni mazito kuhusu suala la maudhui, asilimia 91 ya wananchi wanakubali kuwa mchakato wa kuunda katiba pamoja na maudhui ya katiba vyote ni muhimu. Asilimia 18 wanakumbuka kushiriki katika mchakato wa mapitio ya katiba, asilimia 44 wanaona kuwa mchakato huo ulikuwa kwa ajili ya kukusanya maoni ambayo haikuwa lazima yajitokeze kwenye katiba, na asilimia 23 wanaona kuwa mchakato huo ulikuwa ni kwa ajili ya kuwapa tu taarifa na siyo kukusanya maoni yao. Asilimia 33 waliosalia wanauona mchakato wa katiba kuwa kwa ajili ya kusikiliza maoni ya wananchi na kuyatumia kwenye rasimu za katiba.

Kwa kuongezea, japokuwa asilimia 93 ya wananchi wameshawahi kusikia kuhusu katiba, ni asilimia 35 ya wananchi wanaoweza kueleza maana ya katiba. Asilimia 49 wanasema kuwa Rais ndiye anayepaswa kuongoza mchakato wa kuibadilisha katiba. Kwa ujumla wanawake wana uwezekano mdogo kuliko wanaume wa kufahamu kuwa mchakato wa kuibadilisha katiba ulianza (asilimia 81 ya wanaume ukilinganisha na asilimia 61 ya wanawake) na kwamba walishiriki kutoa maoni yao kwenye mchakato huo (asilimia 25 ya wanaume ukilinganisha na asilimia 10 ya wanawake).

Asilimia 23 ya wananchi waliunga mkono kugomewa kwa Bunge Maalumu la Katiba kulikochochewa na kuanzishwa kwa UKAWA (Umoja wa Katiba ya Wananchi). Idadi muhimu ya wananchi (asilimia 41) wanasema kuwa mgomo huo ulibatilisha mchakato wote, lakini asilimia 56 hawakubaliani na hoja hiyo. Ila, wananchi walipoulizwa kuhusu suala hilo kwa kutumia kauli ya jumla (iwapo kikundi kikiamua kutoshiriki, itasababisha katiba kukosa uhalali), idadi kubwa zaidi ya wananchi (asilimia 56) walikubali.

Katika kusonga mbele, asilimia 48 wanasema njia nzuri ni kuanza upya mchakato wa katiba. Pendekezo la wananchi linalofuata na lililoungwa mkono na asilimia 18 ya wananchi ni kutumia rasimu iliyoandaliwa na tume iliyopita na kuifanyia marekebisho. Kwa upande mwingine, asilimia 38 wanataka mchakato uanze upya kabisa katika ukurasa mpya, wakati asilimia 31 wanataka uanze kwa kutumia rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Asilimia 16 ya wananchi wanataka mchakato uanze kwa kutumia katiba iliyopo hivi sasa na asilimia 11 wangependa itumike rasimu iliyotengenezwa na Bunge Maalumu la Katiba. 

Endelea kusoma: katiba

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

Sehemu