Hawashikiki? Mitazamo na maoni ya Watanzania juu ya rushwa

Benki ya taarifa 21 Nov 2017 hot | Maji & Usafi wa Mazingira

Wananchi wanaripoti kuwa viwango vya rushwa vimepungua nchini. Mwaka huu wa 2017, ni asilimia 85 ya wananchi walioripoti hivo ukilinganisha na mwaka 2014 ambapo asilimia 78 walisema viwango vya rushwa vilikuwa vikubwa kuliko miaka 10 iliyopita.

Wananchi pia wanaripoti kuwa uzoefu wao wa kuombwa rushwa umepungua katika sekta zote mwaka 2017 ukilinganisha na mwaka 2014.

Wananchi wanaripoti kuombwa rushwa na wafuatao:

Polisi: 60% mwaka 2014 na 39% mwaka 2017

Maji: 20% mwaka 2014 na 6% mwaka 2017

Ardhi: 32% mwaka 2014 na 18% mwaka 2017

TRA: 25% mwaka 2014 na 5% mwaka 2017

Afya: 19% mwaka 2014 na 11% mwaka 2017

NGOs: 13% mwaka 2014 na 6% mwaka 2017


Sekta pekee ambayo rushwa iliripotiwa kubaki vilevile ni sekta ya ajira. Asilimia 34 ya Wananchi waliripoti kuombwa rushwa mwaka 2014 huku asilimia 36 wakiombwa rushwa mwaka 2017.

Pengine kutokana na uzoefu wa viwango vikubwa vya rushwa, wananchi wengi wamepata matumaini juu ya mapambano dhidi ya rushwa; mwaka 2014, nusu ya wananchi (asilimia 51) walisema rushwa haiwezi kupunguzwa nchini, wakati mwaka 2017, asilimia 63 ya wananchi wanasema itaweza kupunguzwa kwa kiwango fulani.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kupitia utafiti wake uitwao: Hawashikiki? Mitazamo na maoni wa Watanzania juu ya rushwa. Utafiti huu unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi. Matokeo hayo yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,705 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye utafiti huu) kati ya mwezi Julai na Agosti mwaka 2017.

Pamoja na mtazamo wa wananchi wa kwamba rushwa imepungua, sekta za polisi na mahakama bado zinaongoza kwa rushwa. Asilimia 39 na asilimia 36 ya wananchi wanasema waliombwa rushwa mara ya mwisho walipokutana na taasisi hizo mbili.  Hata hivyo, asilimia 20 ya wananchi wanasema waliombwa rushwa mwaka 2017 kwenye sekta zingine ikiwemo sekta ya ardhi (asilimia 18), afya (asilimia 11) na maji (asilimia 6).

Maelezo ya wananchi ya maana ya rushwa ni: utoaji wa fedha wakati wa kampeni (asilimia 93), utoaji wa fedha/vitu kwa ajili ya kupata huduma (asilimia 78) na kuwalipa wafanyakazi hewa (asilimia 65). Nusu ya wananchi (asilimia 51) wanasema posho za vikao ni rushwa, lakini ni asilimia 3 tu wanaosema wafanyabiashara kutoa fedha kusaidia kampeni za uchaguzi na kisha kutarajia msaada ni rushwa.

Walipoulizwa kuhusu sehemu za kuripoti vitendo vya rushwa, asilimia 56 walizifahamu: Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) (ilifahamika na asilimia 42), polisi (asilimia 10), na mamlaka za vijiji/mtaa (asilimia 4). Ufahamu huu ni kubwa kuliko ule wa mwaka 2014: asilimia 44.

Wananchi wengi wanataka wanaopatikana na hatia ya rushwa wafungwe gerezani. Hii ni adhabu iliyochaguliwa zaidi kwa askari wa barabarani aliyechukua rushwa ya shilingi za Kitanzania 20,000 (asilimia 39); afisa ardhi wa serikali za mtaa aliyechukua rushwa ya shilingi za Kitanzania milioni 5 (asilimia 51) na mwanasiasa mwandamizi wa taifa aliyeiba shilingi za Kitanzania milioni 100 (asilimia 49). Asilimia 30 wangependa afisa wa polisi afutwe kazi kabisa na mwanasiasa arudishe fedha (asilimia 31).

Kashfa za rushwa, ufisadi na ubadhirifu mkubwa hutawala vichwa vya habari na wananchi wengi wanasema rushwa kubwa zipewe kipaumbele katika mapambano dhidi ya rushwa (asilimia 57) ukilinganisha na rushwa ndogo ndogo (asilimia 43). Wananchi wengi wamesikia kuhusu madai ya kesi za rushwa kubwa, lakini ni wachache wanaoweza kuzielezea kwa kina:

Wanaume wa mjini ndio wenye uwezekano mkubwa wa kuwa na taarifa kuhusu kesi hizi.

Tukiangalia madai ya kashfa za rushwa za hivi karibuni, wananchi wengi wanasema serikali ilishughulikia kesi ya Acacia (asilimia 84) na kesi ya TRA/ukwepaji kodi bandarini (asilimia 67) vizuri. Hata hivyo, wananchi wachache wanasema kesi ya Escrow pia ilishughulikiwa vizuri (asilimia 38). Katika kesi mbili za mwanzo, zote ziliibuliwa na serikali lakini kashfa ya Escrow iliibuliwa na vyombo vya habari na vyama vya upinzani. Kwa upande mwingine, mwananchi 1 kati ya 5 (asilimia 18) anasema upinzani ungefanya kazi nzuri ya kupambana na rushwa iwapo ungeshika madaraka.

Mnamo mwezi Septemba 2016, serikali ilianzisha Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa ajili ya kushughulikia kesi kubwa za rushwa na asilimia 32 ya wananchi wamesikia kuhusu mahakama hii. Baada ya kuelezewa kuhusu mahakama hii, asilimia 68 walisema kwamba itafanya kazi kwa ufanisi. Mahakama hii ni sehemu muhimu ya mkakati wa serikali wa kupambana na rushwa. Hata hivyo, wananchi wamegawanyika juu ya rushwa kushughulikiwa vizuri kwa kuwaadhibu waliofanya vitendo hivyo (asilimia 53) au kwa kuvizuia vitendo hivyo visifanyike (asilimia 47).

Wananchi wapo tayari kujitolea ili kupunguza rushwa: asilimia 81 wanakubali kuwa ni muhimu kupambana na rushwa hata kama itachelewesha maendeleo wakati asilimia 19 wanasema tusiwe wakali sana kwa kuwa itaathiri uchumi. Pamoja na hilo, idadi kuwa ya wananchi wanataka itumike njia sahihi katika mapambano dhidi ya rushwa: asilimia 65 wanasema kuwa kila mtu anapaswa kupewa fursa ya kujitetea wakati asilimia 35 ya wananchi wanasema haki za msingi za mtuhumiwa zinaweza kuwekwa kando. 

Endelea kusoma:

featured

pakua nyaraka

Tafsiri

4959 Maoni | Iliyowasilishwa na Jane Shussa (kupitia Risha Chande)

unaweza pia kupenda...