Twaweza.org

Maoni ya wananchi kuhusu ushiriki, maandamano na siasa nchini Tanzania

Wanapotathmini viashiria mbalimbali vya demokrasia, wananchi wengi wanasema uhuru umepungua katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita. Wananchi wanasema uhuru umepungua kwa vyama vya upinzani kufanya mikutano na kutoa maoni yao (64%), vyombo vya habari kukosoa au kuripoti maovu ya serikali (62%), na makundi yasiyofungamana na upande wowote kupaza sauti zao na kufanya mikutano (58%). Nusu ya wananchi pia wanaona hawana uhuru wa kuonesha mitazamo yao ya kisiasa (54%). Uungaji mkono wa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi umeendelea kuwa mkubwa; wananchi karibu 9 kati ya 10 (84%) wakichagua kuwa na vyama vingi vya siasa.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye tatifi zake mbili ziitwazo: Nahodha wa meli yetu wenyewe? Maoni ya wananchi kuhusu ushiriki na maandamano na Tuwapashe Viongozi? Maoni ya wananchi kuhusu siasa nchini Tanzania. Tafiti hizi zinatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mkononi. Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,241 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara mwezi Aprili mwaka 2018 (Zanzibar haihusiki kwenye utafiti huu).

Wananchi wanataka uwazi zaidi kwenye uwajibikaji ambapo asilimia 59% ya wananchi wanataka Rais awajibishwe na Bunge kutoa maelezo ya matumizi ya fedha za walipa kodi, na wananchi wengi zaidi (78%) wanataka Rais aheshimu sheria na maamuzi ya mahakama.

Uungaji mkono wa haki za vyama vya upinzani nao pia umeongezeka. Asilimia 37 ya wananchi wanasema vyama vya upinzani vinapaswa kuikosoa na kuifuatilia serikali ili kuiwajibisha mara baada ya vipindi vya chaguzi kuisha ukilinganisha na asilimia 20 tu walisema hivyo mwaka 2016. Na wananchi wengi zaidi wanasema vyama vya upinzani viruhusiwe kufanya mikutano mwaka huu (64%) ukilinganisha na mwaka 2016 (51%). Kuhusu suala la kukataza maandamano na mikutano ya vyama vya upinzani, wananchi 5 kati ya 10 wanapinga katazo hilo (48%) huku 4 kati ya 10 wakiunga mkono (40%).

Wananchi wenyewe wanasema wako tayari kuchukua hatua za kuiwajibisha serikali ikiwemo kuungana na wengine kuibua hoja (97% wako tayari) na kuzungumza na vyombo vya habari (89% wako tayari) japokuwa kwa mwaka uliopita ni wananchi wachache mno waliofanya hivyo (44% walijiunga pamoja, 5% waliongea na vyombo vya habari). Hata hivyo, wananchi 7 kati ya 10 (71%) walihudhuria mikutano ya serikali mwaka uliopita. Wananchi wanaona kuhudhuria kwenye mikutano ya kufanya maamuzi kama njia nzuri ya kuchangia maamuzi na utekelezaji wa serikali (53%).

Linapokuja suala la kuchukua hatua kubwa, wananchi wachache sana walionesha utayari wa kufanya hivyo. Mwananchi mmoja kati ya wanne (27%) wanasema wangekuwa tayari kushiriki kwenye maandamano kuhusu jambo wasilolipenda huku 65% wakisema hawako tayari, hii ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuliko mwaka 2016 ambapo 50% hawakuwa tayari kushiriki kwenye maandamano. Hamna tofauti kubwa kwa kuangalia kigezo cha umri, jinsia au maeneo lakini hata hivyo wafuasi wa vyama vya upinzani wana uwezekano mara mbili zaidi (45%) wa kushiriki kwenye maandamano kuliko makundi mengine. Sababu kuu iliyotolewa ya kutotaka kushiriki kwenye maandamano ni hofu ya vurugu na kuhatarisha amani (44%).

Pamoja na kutokuwa tayari kushiriki kwenye maandamano, wananchi walizungumza kwa uwazi kuhusu maandamano yaliyopangwa kufanyika Aprili 26 mwaka 2018. Hii inaweza kuangaliwa vizuri kwa kulinganisha takwimu zilizokusanywa kwenye kipindi yalipopangwa maandamano ya UKUTA mwaka 2016. Asilimia 25 ya wananchi walikuwa wanafahamu kuhusu maandamano yaliyopangwa kufanyika Aprili 26, wakati asilimia 19 walikuwa wanafahamu kuhusu UKUTA mwaka 2016. Baada ya maelezo kuhusu maandamano kutolewa, karibu nusu ya wananchi (42%) waliunga mkono maandamano ya Aprili 26 ukilinganisha na 19% waliounga mkono maandamano ya UKUTA. Na mwisho, wananchi 2 kati ya 10 walisema walikuwa tayari kushiriki kwenye maandamano ya Aprili 26 ukilinganisha na mwananchi 1 kati ya 10 kwa maandamano ya UKUTA (19%).

Pamoja na kutokuwa tayari kuandamana na kususia kulipa kodi, wananchi wanaonesha kupunguza imani yao kwa viongozi waliowachagua. Tangu mwaka 2016, uungwaji mkono wa viongozi wote waliochaguliwa umekuwa ukishuka. Ukilinganisha mwaka 2016 hadi 2018, 78% waliunga mkono viongozi wa vijiji ukilinganisha na 56% hivi sasa, mabalozi wa kata walikuwa wakiungwa mkono kwa 74% mwaka 2016 ukilinganisha na 45% mwaka 2018, na viwango vya kukubalika kwa wabunge navyo vimeshuka kutoka 68% hadi 44%. 

Kwa upande wa Rais uungwaji mkono umeserereka kutoka 96% mwaka 2016, ambavyo vilikuwa ni viwango vya juu kuwahi kutokea nchini, mpaka 55% mwaka 2018, viwango vya chini kabisa kuwahi kutokea kwenye historia ya nchi. Pamoja na hilo, wananchi kwa kiasi kikubwa wanaendelea kuwaunga mkono wagombea wa CCM. Zaidi ya nusu wangewapigia kura wagombea wa CCM wa udiwani (51%), wabunge (51%), na Urais (55%).

Uungwaji mkono wa CCM kama chama umeendelea kuwa imara kiasi kwenye miaka ya hivi karibuni kukiwa na 63% ya wananchi wanaosema wako karibu na CCM mwaka 2017 ukilinganisha na 58% mwaka 2018. Hata hivyo, uungwaji mkono wa CCM umeshuka zaidi kwenye maeneo ya vijijini ikiwa na maana kwamba sasa chama hicho kinaungwa mkono kwa kiwango sawa katika maeneo ya vijijini (59%) na mijini (56%). Uungwaji mkono wa Chadema nao pia umeshuka, kutoka 25% mwaka 2015 hadi 16% mwaka 2018. Idadi kubwa inayoongezeka ya wananchi hawako karibu na chama chochote cha siasa (17% mwaka 2017, 24% mwaka 2018. 

Endelea kusoma:

featured

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri