Twaweza.org

Tukiwathamini walimu, lengo la elimu bora litatimia

Makala hii imeandikwa na Greyson Mgoi, Ofisa mawasiliano wa Uwezo iliyoko Twaweza na kuchapishwa katika gazeti la Mwananchi. 

HISTORIA inabainisha kuwa miaka ya 1970 serikali ya Tanzania iliweka mikakati ya utekelezaji wa sera ya elimu kwa wote “Universal Primary Education (UPE)”, sera iliyopitishwa mwaka 1974 na ilianza kutekelezwa 1977.

Lengo lilikuwa kuchochea kasi ya maendeleo kupitia mpango kamambe wa kufuta ujinga, umasikini na maradhi katika Tanzania huru. Wakati huo walimu walipewa nafasi muhimu sana katika maendeleo ya taifa letu na pia waliheshimika na kuthaminika hata kwa jamii zinazowazunguka na kuonekana ni watu wa maana kwelikweli.  

Aidha kutokana na matatizo mbalimbali ikiwemo kupuuzwa kwa walimu, miaka ya 1980 hadi 1990, jamii ilishuhudia kuporomoka kwa ubora wa elimu kwa kasi kubwa sana, jambo ambalo lilipelekea serikali kuanzisha mpango kamambe wa kuinua sekta ya elimu kupitia sera ya kupunguza umaskini.

Ndipo ulianza utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi (MMEM) mwaka 2001. Pamoja na kauli nzuri zilizokuwa zikitolewazo na kila mdau wa elimu mfano kauli kuwa, walimu ni muhimu katika utoaji elimu bora, bado walimu waliendelea kutokupewa kipaumbele katika utekelezaji wa mipango ya elimu.

Walimu waliendelea kuishi na kufanya kazi katika mazingira magumu sana. Mfano, nyumba za kuishi zenye hadhi duni kabisa, ufinyu wa mishahara yao, kutopewa maslahi yao stahiki kisheria kama vile, malipo ya uhamisho na likizo, na hata posho nyingine mbali mbali.

Toka wakati huo mpaka sasa hapa ndipo tulipofikia, licha ya mchango mkubwa wanaoutoa kwenye jamii, walimu bado wanachukuliwa kama watu wa kada ya chini, isiyo na thamani katika jamii ukilinganisha na kada nyingine kama uuguzi, udaktari, uaskari na nyingine kama hizo.

Inashangaza kuona jamii ya sasa inamchukulia mwalimu kama mtu aliyeshindwa kufanya/kupata kazi nyingine ndio akakimbilia ualimu. Mwalimu ni mtu anayetafsiriwa kuwa anaishi maisha ya duni, ya kubangaiza huku akisongwa na madeni lukuki. Msakatonge.

Inastaajabisha sana kuona jamii ambayo watoto wao wanapata elimu kutoka kwa walimu hao hao na badae wanakuwa wasomi wazuri na kupata kazi nzuri, ndio hao hao wamekuwa wakiwadharau walimu na kuwaona ni kundi la watu walioshindwa maisha.

Aidha walimu mbali na kudharauliwa na baadhi ya watu katika jamii, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingine nyingi sana wakati wakitekeleza majukumu yao.

Utafiti uliyofanywa na Twaweza kupitia jitihada yake ya Uwezo Tanzania hapo mwaka 2015 na matokeo yake kuzinduliwa mwaka 2017, unaonesha kuwa wastani wa uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi kitaifa ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 44. (1:44). Wilaya yenye uwiano mzuri ina mwalimu mmoja kwa wanafunzi 25 wakati wilaya yenye uwiano  duni ina mwalimu mmoja kwa wanafunzi 75. Takwimu hizi ni kwa wilaya za Tanzania bara.

Hapo utaona namna gani walimu wengi ambavyo bado wanamzigo mziti wa kuhudumia rundo la wanafunzi katika chumba kimoja cha darasa huku wakilazimika kuhakikisha wanafunzi hao wote wanasoma na kupata maarifa kamili yaliyo kusudiwa ili lengo la kuwapatia elimu bora watoto wote kwa usawa litimie.

Changamoto nyingine wanayokumbana nayo walimu i kufundisha watoto wenye njaa.

Mfano takwimu za Uwezo zinaonesha kuwa  kwa wastani kitaifa ni  shule 2 tu kati ya10 ( 24%)  ndio zinatoa chakula cha mchana kwa wanafunzi. Kwa maana hiyo, watoto wengi wanasoma wakiwa na njaa!

Hali hii ya kuhudhuria masomo wakiwa na njaa inawafanya watoto wengi kusoma katika mazingira magumu na inaathiri matokeo ya kujifunza kwa mtoto. Ambapo matokeo ya kujifunza yakiwa mabaya mwalimu ndiye ambaye siku zote hulaumiwa kwa kutotimiza majukumu yake barabaraa.  

Tarehe 5 Mwezi  Oktoba kila mwaka, dunia huadhimisha siku ya walimu, ambapo lengo huwa ni kuthamini na kutambua mchango wa walimu katika jamii zetu na katika maendeleo ambapo kimsingi walimu ndio wametufanya kama dunia kwa ujumla tufikie hapa tulipo sasa kimaendeleo.

Pia tukiadhimisha siku hii muhimu, shughuli nyingi hufanywa na wadau mbalimbali wakilenga kukuza uelewa wa jamii iweze kutambua na kuthamini juu ya nafasi muhimu ya mwalimu katika jamii zetu.

Siku ya Mwalimu duniani ilianza kuadhimishwa rasmi hapo mwaka 1994 na jitihada iliyoanzishwa na shirika la Elimu la kimataifa (UNESCO). 

Toka wakati huo siku hii imekuwa ikiadhimishwa kila mwaka na wadau sehemu mbalimbali duniani ambapo wengi wameitumia siku hii kukumbuka, kuthamini, kutambua mchago mkubwa wa walimu katika maendeleo.

 Mwaka huu tunapo adhimisha siku hii muhimu, rai yangu kwa jamii ya watanzania ni kuwa kila mmoja popote alipo athamini mchango wa walimu, awashukuru na kuwapongeza walimu, pia ashirikiane kikamilifu na walimu katika masuala ya elimu mara kwa mara.

Kwa kufanya hivyo walimu watakuwa na motisha, ari yao ya kufundisha itapanda zaidi na hakika watoto wetu watapata  elimu bora na dunia itaweza kufikia kutimiza lengo namba nne la malengo endelevu ya dunia (SDG4) ambalo linakusudia kila mtoto duniani apate elimu bora. Mimi nawathamini na kuwapongeza walimu wangu kwa kazi nzuri waliyofanya kwangu mpaka nimefika hapa,wewe je?

Endelea kusoma: elimu

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri