Twaweza.org

Tunachotaraji Kufanikisha

Tunachotaraji kufanikisha

Mabadiliko ya kweli huchukua muda. Si lengo letu kukurupuka na mambo mepesi mepesi na kisha kuweka tiki katika mabano ya ufanisi. Ndiyo maana Twaweza imejipangia kipindi cha miaka kumi, ikiwa na malengo mawili. Kwanza, tunataka kuimarisha ‘utashi wa wananchi’ kwa maana ya uwezo wa wanaume, wanawake na vijana kupata taarifa zilizo bora na za kuaminika, kwa haraka zaidi na kwa bei nafuu; waweze kufuatilia na kujadili kinachoendelea, waweze kusema kwa uwazi na wachukue hatua kuleta mabadiliko. Hii peke yake ni muhimu, kwa sababu kila mtu anatakiwa ajisikie kwamba anao uwezo au udhibiti juu ya maisha yake. Lakini pia ni muhimu kwa sababu inashadidia lengo letu la pili, ambalo ni kuwawezesha watu wengi zaidi kujipatia huduma bora za elimu, afya na maji safi. Kazi yenyewe imepangwa kwa ajili ya kipindi cha miaka kumi, na itatathminiwa kwa uangalifu na kitengo huru kutoka nje.

Matokeao ya Utashi wa wananchi (2013)

Katika miaka mitano ya kwanza, Twaweza inatafuta kuongeza upatikanaji wa habari kwa wananchi kuhusu huduma na stahili zao, kukuza fursa za wananchi kueleza maoni yao hadharani na kulea utamaduni ambamo wananchi wanafuatilia serikali, rasilimali za umma na utoaji wa huduma kwa karibu. Aidha tunakusudia kusaidia kuinua ubora wa vyombo vya habari na kuongeza wingi wake kote Afrika Mashariki. Kupitia juhudi hizi tunataraji kuona wananchi wakijenga uelewa mkubwa zaidi wa uwezo wao wa kusababisha mabadiliko – huuu ndio tunauita utashi wa wananchi

Matokeo ya upatikanaji wa huduma (2018)

Tunaamini kwamba kadri  wananchi wanavyokuwa werevu, wakajishughulisha zaidi na wakawezeshwa zaidi ndivyo watakavyoweza kudai uwajibikaji mkubwa zaidi na huduma zilizoboreshwa. Ifikapo mwaka 2018, Twaweza inahitaji kuona mabadiliko katika matokeo yaliyoboreshwa katika elimu, huduma za afya na maji. Katika elimu tunataraji kuona walimu wengi zaidi wakienda kufundisha madarasa yao, fedha nyingi zaidi zikizifika shuleni na zikitumiwa ipasavyo na watoto wengi zaidi wakiweza kusoma na kuandika vizuri zaidi. Kuhusu maji, Twaweza inalenga upatikanaji wa maji safi na kupunguza hatari zitokanazo na maji pamoja na magonjwa yaenezwayo kwa maji. Katika afya tunalenga kuona watumishi wengi zaidi wa sekta hii wakienda kufanya kazi zao za kutoa huduma za afya, upatikanaji mkubwa zaidi wa madawa ya msingi na huduma ya chanjo DPTHb3, yote yakiashiria hali ya siha njema katika jamii. Ili kupata taswira nzuri zaidi ya jinsi mabadiliko hayo yanavyoweza kuwa, angalia hapa.

Matokeo  ya Kujifunza

Twaweza inakuza utamaduni wa kujifunza miongoni mwa wafanyakazi wake na miongoni mwa wabia wake kwa ujumla. Tutawezesha mahusiano ya ufundishaji na ufuatiliaji kuwahamasisha wabia wetu watafakari kuhusu kazi zao ili waweze kuziboresha. Kitengo huru chenye mahusiano ya chuo kikuu kimekwisha kuandaliwa ili kifanye tathmini ya kazi yetu kwa kipindi cha miaka mitano ijayo na kihakiki mabadiliko tangu mwanzo. Tutaidurusu miardi yetu kwa karibu sana na tuweke nyaraka kuhusu nini kinafaa na kipi hakifai, tukizalisha nyaraka za ushahidi na ujuzi mpya na kisha tuweza kuchangia taarifa zetu kwa upana mkubwa, na hivyo kuongeza ubora ndani ya Twaweza na hata nje yake.

Endelea kusoma: malengo ya Twaweza

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri