Twaweza.org

Tunavyofanya kazi

Twaweza inakusudia kukuza “miundo-hali ya mabadiliko” kwa kujenga juu ya msingi wa kazi za wananchi kuleta mabadiliko, au kuchochea kazi hizo na kuziimarisha kwa kujenga ubia na ushirika.

Katika kila kijiji na kila mtaa wa mji, wananchi wa kawaida wanachambua, wanapanga na kuchukua hatua juu ya masuala yaliyo muhimu kwao. Mara nyingi juhudi zao huzaa mabadiliko muhimu, lakini juhudi hizi huathiriwa na kukosekana kwa taarifa muhimu kuhusu serikali yao na jumuiya yao. Kw a hiyo wananchi wengi hushindwa kuwa na msimamo maridhwa pale serikali au asasi nyingine husika zinaposhidnwa kutoa huduma au kutumia rasilimali vyema. Wananchi wanapokuwa na uwezo wa kupata taarifa, huduma ya vyombo vya habari na huduma nyingine, wanakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kujipatia huduma bora na kufutailia maslahi yao. Kwa kukuza ubia unaoweza kujenga nyenzo na rasilimali hizi, Twaweza inaunga juhudi za wabia katika kuimarisha juhudi zilizopo na kuibua nyingine mpya. Tunaamini kwamba hii itasaidia kujenga wananchi wenye ari kubwa zaidi ya kutenda, jamii zenye uwezo mkubwa na serikali zinazowajibika zaidi.

Mtazamo wa Twaweza ni kuanza na wananchi wenyewe na mitandao ambayo tayari ni muhimu kwao, na kubuni mbinu mwafaka za kuwawezesha wananchi wa kawaida kwa mamilioni wanaweza kuchukua hatua kuleta mabadiliko. Twaweza si asasi ya utekelezaji, na wala si chombo cha ufadhili kwa miradi inayoonekana mizuri, bali kazi yetu ni kukuza uibuaji wa fikra mpya na majaribio, na kujenga mikakati ya ubia inayoweza kuleta mabadiliko makubwa nchini kote, na kufanya tathmini ya mchakato huo.Kila ubia unajengwa kwa madhumuni ya kufanikisha lengo mahsusi lenye maana halisi kwa wananchi wa kawaida – kama vile kuhakikisha kwamba fedha zinafika shuleni na zinatumika kama zilivyokusudiwa, vituo vya maji vinafanya kazi kuwahudumia masikini, au kuboresha upatikanaji wa chanjo.

Ubia huo unahusisha asasi zenye uwanda mpana wa mahusiano miongoni mwa jamii na zina umuhimu katika maisha ya wananchi, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari, kampuni za simu za mkononi, mitandao ya biashara, asasi za kidini na vyama vya wafanyakazi. Badala ya kujaribu kujenga mtandao mpya kabisa wa usambazaji, Twaweza itajitahidi ‘kupandia’ mitandao hii ambayo tayari ipo. Tutajaribu kutambua malengo yanayoshabihina kati ya wabia, ili kuyafanyia kazi kwa pamoja, badala ya kutafuta kupewa hisani.Tutayafanyia kazi na kujenga juu ya yale maeneo ambayo wabia wenyewe wanayamudu vyema, tukielewa vyema kwamba ubia unakuza maslahi binafsi ya mbia, na kwa gharama nafuu, na wakati huo huo ukisaidia kukidhi maslahi ya jamii. Kwa kukusanya pamoja nguvu za wabia katika jitihada zilizounganishwa, huu ubia utaweza kuwafikia mamilioni ya wananchi katika eneo hili na kuwawezesha kutumia mitandao hii kuleta mabadiliko.

Endelea kusoma: maadili ya kazi

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri