Twaweza.org

Wadau waitaka serikali kutekeleza Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa

Duniani kote, sheria za upatikanaji wa taarifa zimebadilisha uhusiano uliopo kati ya wananchi na serikali. Wananchi wanapoelewa serikari yao inafanya nini, huweza kuchagiza maendeleo na wao wenyewe kunufaika. Wananchi wakiwa na taarifa za kutosha huweza kuchangia ipasavyo jitihada mbali mbali za maendeleo zenye kuleta maboresho ya jamii. Wakati mwingine, wanaweza kusaidia kufichua vitendo vya rushwa na uovu katika jamii zao. Mara nyingi upatikanaji wa taarifa huiwezesha serikali kuhakikisha mipango yake inaendana na hali halisi ya jamii. Pia taarifa huwasaidia watafiti kuchunguza zaidi na kutoa ufumbuzi wa matatizo sugu yanayozikabili jamii.  

Wananchi huweza kuuona umuhimu wao pale wanapoweza kufuatilia yale yanayoendelea katika jamii zao, na kuyachukulia hatua. Jamii bora ni ile inayoendesha shughuli zake kwa uwazi, ushirikishwaji na uwajibikaji; na yenye mifumo ya kuwapatia wananchi taarifa kwa uharaka. Jamii kama hiyo huwapa wananchi nafasi ya kushiriki kwenye masuala ya kijamii na huwapa nafasi za kutoa mawazo yao kwa uhuru, na demokrasia ya kuchagua viongozi wao na kuwawajibisha.

Sisi, wanachama wa umoja wa AZAKI zinazojishughulisha na masuala yahusuyo haki ya kupata taarifa, (Coalition on the Right to Information) tunaipongeza serikali kwa mara nyingine kwa kupitisha Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa (2016), hususani kwa kuthamini mawazo na maoni ya baadhi ya wadau kabla ya sheria hiyo haijapitishwa.

Hata hivyo, inasikitisha kuwa kanuni zinazoratibu utekelezaji sheria hii bado hazijaandaliwa, na pia kwamba sheria hii bado haijatangazwa rasmi katika gazeti la serikali. Sheria hii ilipitishwa mwaka mmoja uliopita lakini mpaka sasa bado haijaanza kutumika.

Katika kuelekea Siku ya Kimataifa ya Upatikanaji wa Taarifa (Septemba 28), tunaiomba serikali ianze hatua ya majadiliano ya kuandaa kanuni ili zikamilishwe mapema iwezekanavyo. Kwa sasa, tunaomba serikali itangaze sheria hii kwenye gazeti la serikali wakati mchakato wa kuaandaa kanuni unaendelea.

Kwa sasa, kuna uwezekano mkubwa kwamba wananchi hawapati taarifa pindi wanapozihitaji. Mwezi Januari/Februari mwaka 2016, watafiti, wakiwa kama wananchi wa kawaida, walitembelea ofisi 131 za serikali. Ofisi hizi zilikuwa katika wilaya 26 na takwimu zilizokusanywa zina uwakilishi wa kitaifa.

Nia ya ziara hizi ilikuwa kutafuta taarifa fulani na watafiti hao walifanikiwa kupata taarifa za suala 1 kati ya masuala 3 (asilimia 33) waliyokuwa wanayahitaji. Hii inamaanisha kuwa, wananchi hawapati taarifa juu ya masuala mawili kati ya matatu wanayoyahitaji, kutoka katika ofisi za serikali. Japokuwa takwimu hizi zilikusanywa kabla ya kupitishwa kwa Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa, hakuna sababu ya kudhani kuwa matokeo haya yamebadilika kwa kiwango kikubwa.

Kutokana na utafiti uliopita, tungependa kujikita kwenye maeneo yafuatayo: 

  • Asilimia 84 ya wananchi waliunga mkono mswada wa upatikanaji wa taarifa bungeni kabla haujapitishwa kuwa sheria, hii inaonesha kuwa wananchi wangependa kupata taarifa za serikali.
  • Asilimia 77 ya wananchi wanaamini kuwa wananchi wa kawaida wanapaswa kupata taarifa zinazomilikiwa na serikali.
  • Asilimia 80 ya wananchi wanaamini kuwa rushwa na matendo mengine maovu yatapungua iwapo wananchi watakuwa na uwezo wa kupata taarifa.
  • Asilimia 42 ya wananchi wangependa kupata taarifa zaidi zinazohusu sekta mbalimbali kutoka serikalini. 

Soma zaidi hapa.

Endelea kusoma: access to information

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri