Uwezo Tanzania | Ukosefu wa usawa katika elimu
27 Feb 2018
hot
|
Matangazo

Miongoni mwa watoto wenye umri wa miaka 9 hadi 13, asilimia 38 hawawezi kufanya majaribio ya darasa la 2 huku tofauti kubwa ikionekana kwenye wilaya. Wilaya ya Iringa Mjini, inayoongoza kwa ufaulu, asilimia 75 ya watoto wenye umri wa miaka 9 hadi 13 wana uwezo wa kufaulu majaribio ya kusoma Kiingereza na Kiswahili na kufanya hesabu za darasa la pili. Lakini wilayani Sikonge ni asilimia 17 tu ya watoto walioweza kufaulu majaribio hayo.
Asilimia 64 ya watoto mkoani Dar es Salaam wenye miaka 9 hadi 13 wana uwezo wa kufaulu majaribio yote matatu, lakini mkoani Katavi, ni asilimia 23 tu ya watoto wanaoweza kufaulu majaribio hayo. Aidha, watoto wawili kati ya kumi (asilimia 16) wenye umri wa miaka 11 wako nyuma kimasomo mkoani Dar es Salaam. Mkoani Katavi, idadi hiyo ni watoto saba kati ya kumi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze anasema “takwimu hizi za Uwezo zinaonesha kuwa maeneo wanapoishi watoto yana mchango mkubwa katika kujifunza kwa watoto hao kuliko umasikini, kiwango cha elimu ya mama, iwapo mtoto amesoma shule ya awali au hata watoto wenye udumavu. Ukweli huu ni changamoto kwa watunga sera kuelekeza juhudi na rasilimali kwenye wilaya au sehemu hizi.”
Matokeo haya yametolewa na Uwezo Tanzania iliyoko Twaweza kwenye ripoti iitwayo Je, Watoto Wetu Wanajifunza? Ripoti ya Mwaka 2017 ya Upimaji wa Kujifunza ya Uwezo Tanzania. Ripoti hii inatokana na takwimu zilizokusanywa na Uwezo Tanzania, tathmini kubwa barani Afrika ya kupima matokeo ya kujifunza nchini Kenya, Tanzania na Uganda. Katika awamu ya sita ya ukusanyaji wa Takwimu uliofanywa na Uwezo Tanzana mwaka 2015, jumla ya watoto 197,451 walitathminiwa kutoka kaya 68,588. Takwimu pia zilikusanywa kutoka katika shule za msingi 4,750.
Tofauti kubwa zinabainika pia katika vifaa, rasilimali na huduma zipatikanazo shuleni.
- Mkoani Dar es Salaam, nusu ya shule (asilimia 51) zina huduma ya umeme, lakini mkoani Geita, ni shule 2 tu (asilima 4 tu) kati ya 50 zinazopata huduma hiyo.
- Mkoani Geita, shule moja tu kati ya kumi (asilimia 12) ina huduma ya maji safi na salama, lakini mkoani Kilimanjaro, karibu shule 8 kati ya 10 (asilimia 78) zina huduma hiyo.
- Mkoani Kilimanjaro, wanafunzi 26 wanatumia choo kimoja, ukilinganisha na mkoani Geita ambapo wanafunzi 74 wanatumia choo kimoja.
- Vile vile, asilimia 5 ya shule mkoani Geita zinatoa huduma ya chakula cha mchana wakati mkoani Kilimanjaro ni asilimia 79.
- Mkoa wa Dar es Salaam, wanafunzi sita wanatumia kitabu kimoja wakati mkoani Kilimanjaro, wanafunzi wawili tu wanatumia kitabu kimoja.
- Mkoani Kilimanjaro mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 36, lakini Katavi, mwalimu huyo mmoja anafundisha wanafunzi 52.
Endelea kusoma: Elimu Tanzania
pakua nyaraka
- Inequalities in Education | Presentation |
2.55 MB
- Wilaya wanapoishi watoto zina mchango mkubwa katika kujifunza: tofauti ya ufaulu kati ya wilaya bora na zile za mwisho ni asilimia 60 | Press Release |
162.38 KB
- Where children live matters more than anything else for learning: the gap between the best and worst performing districts is 60 percentage points | Press Release |
167.07 KB
- Inequalities in Education | Agenda |
625.18 KB
Tafsiri
unaweza pia kupenda...
- Serikali na wadau wa Elimu nchini tushirikiane kuboresha matokeo ya kujifunza (19 Apr 2018)
- #ArudiShuleni (3 Jul 2017)
- Elimu inaanzia nyumbani (10 Feb 2012)
- Matokeo ya mtihani wa kumaliza shule ya msingi Kenya yathibitisha matokeo ya Uwezo (20 Jan 2012)
- Mkuu wa Wilaya: wanafunzi 3000 hawajui kusoma Iringa (21 Nov 2011)
- Uwezo Tanzania 2011: Watoto wetu bado hawajifunzi (15 Sep 2011)
- Matumizi ya Kiswahili na Kiingereza: Hugawa Mabataka ya Jamii na Kudororesha Viwango vya Elimu (15 Jul 2011)