Twaweza.org

Dar es Salaam wanachukuliaje utawala?

Wakazi wa Dar es Salaam hawaridhishwi na viwango vya utoaji huduma za jamii, waelezea jinsi rushwa inavyozidi kukithiri na hawana imani thabiti kwa taasisi za umma na viongozi wanaopaswa kuwawakilisha na kuwatumikia. Viwango vya kutoridhishwa na jinsi utoaji huduma za jamii unavyosimamiwa ni vya juu sana. 

Matokeo haya yametolewa kupitia muhtasari wa uchambuzi wa sera uliofanywa na Uwazi—Twaweza  uliopewa jina la Dar es Salaam wanachukuliaje utawala? Maoni ya watu kuhusu huduma, sera na viongozi. Muhtasari huo wa sera umetokana na taftishi iliyoendeshwa katika kaya 550 mwezi Agosti hadi Septemba, 2010. Taftishi hiyo iliendeshwa katika wilaya za Ilala, Kinondoni na Temeke. Wahojiwa waliulizwa maoni yao kuhusu hali ya utoaji wa huduma na jinsi walivyojishughulisha kutatua masuala yaliyowagusa.

Licha ya viwango vya juu vya kutoridhishwa hali ya utoaji wa huduma za jamii na kutokuwa na imani, wakazi wa Dar es Salaam hawakuonyesha, katika taarifa walizotoa, kuwa na ari kubwa ya kuchukua jukumu la kuleta mabadiliko katika matokeo ya utoaji wa huduma. Hofu ya kuadhibiwa huenda ni moja ya sababu. Karibu asilimia 40 ya washiriki wa taftishi walisema wanafikiri kulikuwa na uwezekano wa kuadhibiwa kwa kukemea utoaji wa huduma mbovu. Kwa ujumla, wahojiwa wa taftishi waliripoti kuchukua hatua katika vikundi zaidi kuliko kama mtu mmojammoja. Njia zilizotumika sana katika hili ni kushiriki kwenye mijadala ya mitaani (48%); kushiriki mikutano ya jamii (59%) na mikutano ya kamati za shule (40%). Kwa upande mwingine, ni asilimia 8 tu ya wahojiwa ndiyo waliozungumzia masuala ya jamii kupitia njia za kawaida za mawasiliano na asilimia 10 walipiga simu kwenye vipindi vya redio. Sababu nyingine ni ari ndogo ya kuchukua hatua kushughulikia masuala yasiyoridhisha inaweza kuhusishwa na hali ya wananchi kutojua  njia/fursa na nyenzo zilizopo na zilizo wazi kwao, au ile imani ya kwamba huenda ushiriki wao unaweza usibadilishe chochote.

Mushi Elvis wa Twaweza anaeleza kwamba ‘Utoaji wa huduma ulio duni ni suala ambalo serikali haina budi kulishughulikia kama jambo la kupewa kipaumbele. Hata hivyo, kama raia, tuna haki na wajibu wa kuhakikisha kwamba tunafanya sehemu yetu, kwa kuzisoma na kuzifahamu sera na vipaumbele vya kitaifa, kuweka wazi masuala tunayokabiliana nayo, na kuwasiliana na viongozi na taasisi zinazotuwakilisha ili watambue maoni/mitazamo yetu.’

Endelea kusoma:

Authors: rose aiko

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri