Twaweza.org

Watafiti wa kujitolea elfu nane kutathmini watoto Tanzania Bara

Jumla ya watafiti wa kujitolea 7,980 wanashiriki katika Tathmini ya Uwezo katika wilaya 133 za Tanzania Bara. Utafiti huu unalenga kujua uwezo wa watoto katika kusoma Kiswahili, Kiingereza na kufanya hesabu. Tathmini hii ni jitahada za Uwezo kila mwaka kukagua ubora wa msingi wa elimu kwa watoto.

Uwezo inaamini kuwa msingi wa elimu bora kwa watoto unapatikana kwa watoto kujifunza kwa kiwango na ubora unaotakiwa. Lakini, pamoja na jitihada za Serikali na wadau wengine kuboresha miundombinu na vifaa shuleni pamoja na kuajiri walimu, swali la msingi la kujiuliza ni: Je, watoto wetu wanajifunza?

Tathmini ya Uwezo ni zoezi la kisayansi la nchi nzima linalolenga kukusanya takwimu ili kujua stadi na kiwango cha watoto wetu katika kusoma na kufanya hesabu. Utafiti huu unatathmini watoto kwa kiwango cha mtaala wa darasa la pili. Zaidi ya watoto laki moja na hamsini na tano (155,000) wenye umri wa miaka 7 – 16 watatathminiwa mwaka huu. Watoto hawa wanatoka katika kaya 79,000 zilizomo katika vijiji na mitaa 4,000 nchi nzima.

Sababu ya msingi ya kufanya tathmini hii majumbani ni kutoa fursa kwa wazazi kupata matokeo papo hapo ya tathmini kwa watoto wao ili kujua udhaifu upo wapi na wanawezaje kuwasaidia watoto wao. Katika jamii nyingi zilizofanyiwa utafiti, wazazi wamepata mwamko wa kufuatilia na kusaidia watoto masuala yanayohusu elimu ya watoto wao.

Msingi wa mafanikio bora katika elimu upo katika ngazi ya chini kabisa ya kusoma na kufanya hesabu kwa watoto. Uwezo inaamini - kwamba kushindwa kwa watahiniwa wengi wa sekondari katika ngazi ya Kidato cha Nne kunachangiwa, kwa kiasi fulani, na kukosekana kwa stadi muhimu za kusoma na kufanya hesabu kwa watoto. Hii inasababisha hali ya kufeli kujirudia kadiri watoto wanavyosonga mbele katika elimu ya msingi na sekondari.

Katika utafiti wa mwaka jana, Uwezo iliegundua kuwa ni mtoto 1 tu kati ya watoto 5 wa darasa la tatu 3 anayeweza kusoma na kufanya hesabu kwa kiwango cha darasa la 2.

Soma Taarifa kwa Umma au nakala ya majaribio ya Uwezo

Endelea kusoma: elimu

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri