Twaweza.org

Je, watoto wetu wanajifunza? Tathmini ya sita ya Uwezo Tanzania

Miongoni mwa watoto wenye umri wa miaka 9 hadi 13, wengi wao hawawezi kufanya majaribio ya kiwango cha darasa la 2. Pia kuna tofauti kubwa sana kiwilaya. Iringa Mjini, wilaya iliyofanya vizuri, asilimia 74 ya watoto wenye miaka 9 hadi 13 walifaulu majaribio ya kusoma Kiswahili na Kiingereza na kufanya hesabu. Kwa upande wa wilaya ya Sikonge, ni asilimia 15 pekee waliofaulu. Kimkoa, asilimia 64 ya watoto katika mkoa wa Dar es Salaam wenye miaka 9 hadi 13 walifaulu majaribio yote matatu, lakini katika mkoa wa Katavi asilimia 23 pekee ya watoto wenye umri kama huo ndio waliofaulu.

Vilevile, asilimia 42 kutoka kaya masikini walifaulu majaribio yote matatu ukilinganisha na asilimia 58 kutoka kaya tajiri. Tofauti hizi zinaonesha kuwa mahali anapoishi mwanafunzi panachangia kwa kiwango kikubwa matokeo ya kujifunza kuliko hali ya kiuchumi na vitu vingine ambavyo hudhaniwa kuhusika katika kuleta mafanikio kielimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, anasema “inatia moyo kuona watoto wetu wanapata matokeo mazuri zaidi kuliko miaka ya nyuma kwenye somo la Kiswahili, lakini safari bado ni ndefu. Kitu cha kutia shaka ni ongezeko la kukosekana kwa usawa kwenye matokeo ya kujifunza kutokana na maeneo wanayoishi watoto. Takwimu zetu zinaonesha kuwa mahali anapoishi mtoto huchangia kwa kiwango kikubwa uwezo wake wa kujifunza, kuliko sababu zinginezo kama vile elimu ya mama yake, kupata ama kutokupata elimu ya awali au kuwa na udumavu ama la.”

Matokeo haya yametolewa na Uwezo Tanzania iliyopo Twaweza katika ripoti iitwayo Je, Watoto Wetu Wanajifunza? Ripoti ya Sita ya Mwaka ya Upimaji wa Kujifunza (Kiingereza). Ripoti hii inatokana na takwimu zilizokusanywa na Uwezo Tanzania ambayo ni sehemu ya tathmini kubwa barani Afrika inayopima matokeo ya kujifunza ikiongozwa na wananchi. Tathmini hii pia inatekelezwa nchini Kenya na Uganda. Katika awamu ya sita ya ukusanyaji wa takwimu uliofanywa na Uwezo Tanzania mwaka 2015, jumla ya watoto 197,451 walifanyiwa tathmini kutoka kaya 68,588. Takwimu hizo zilikusanywa kutoka shule za msingi 4,750.

Kwa ujumla matokeo ya kujifunza hayajafikia kwango stahili ukilinganisha na matarajio ya mitaala katika masomo yote matatu. Miongoni mwa wanafunzi wa darasa la 3 na la 7:

  • Wanaoweza kusoma hadithi ya Kiswahili: Darasa la 3 - 56%, Darasa la 7 - 89%
  • Wanaoweza kusoma hadithi ya Kiingereza: Darasa la 3 - 13%, Darasa la 7 - 48%
  • Wanaoweza kufanya hesabu za Kuzidisha: Darasa la 3- 35%, Darasa la 7 - 78%


Hata hivyo yapo matokeo chanya: kati ya mwaka 2011 na 2015 viwango vya ufaulu katika somo la Kiswahili vimeongezeka karibu mara mbili kutoka asilimia 29 hadi asilimia 56 (kwa wanafunzi wa darasa la 3). Kwa darasa la 7, kiwango cha ufaulu kimeongezeka kutoka asilimia 76 hadi asilimia 89 katika kipindi hicho hicho.

Japokuwa bado inaonesha kuwa wanafunzi wengi hasa walio katika madarasa ya chini wapo nyuma ya matarajio ya mtaala, lakini hii inatupa matumaini. Kuna dalili kuwa jitihadi za pamoja za serikali, ikiwemo misaada kutoka kwa wahisani wa maendeleo, za kujikita kwenye kuboresha stadi za msingi katika madarasa ya mwanzo kupitia programu mbalimbali, zinaanza kuzaa matunda.

Vilevile uwiano kati ya wanafunzi na vitabu umeboreka kutoka wanafunzi 30 kutumia kitabu kimoja mwaka 2013 hadi wanafunzi 8 mwaka 2014, mpaka kufikia wanafunzi 3 wanaotumia kitabu kimoja mwaka 2015. Takwimu hizi zinaonesha kiwango cha mabadiliko kinachoweza kufikiwa na hatua imara zinazosimamiwa vizuri.

Kwa upande mwingine, ripoti hii ya Uwezo inaonesha kushuka kwa kiwango cha uandikishwaji wa watoto, hususani vijijini. Mwaka 2011, asilimia 77 ya watoto wenye umri wa miaka 7 waliandikishwa shule ya msingi ukilinganisha na asilimia 55 mwaka 2015. Kwa kuangalia uandikishwaji wa watoto wenye umri kama huo kwenye taasisi yoyote inayotoa elimu (ikiwemo shule za awali), takwimu zimeshuka kutoka asilimia 86 mwaka 2011 hadi 81% mwaka 2015. Uchambuzi wa kina unaonesha kuwa ushukaji huo unajitokeza zaidi kwenye maeneo ya vijijini: uandikishwaji wa watoto wenye miaka 7 kwenye taasisi yoyote inayotoa elimu (ikiwemo shule za awali) umeshuka kutoka asilimia 84 mwaka 2011 hadi asilimia 78 mwaka 2015. Kwenye maeneo ya mijini uandikishaji umeshuka kutoka asilimia 94 (2011) mpaka asilimia 93 (2015). Vilevile, viwango vya uandikishwaji vijijini vinaonekana kushuka miongoni mwa rika zote wakati kwenye maeneo ya mijini umeendelea kuimarika.

Kwa ujumla mwalimu mmoja kati ya wanne (asilimia 25) na karibu wanafunzi watatu kati ya kumi (asilimia 29) hawakuwepo shuleni siku ya tathmini. Hii inaathiri muda wa wanafunzi na mwalimu kukutana na hivyo kupunguza muda wa kufundisha na kujifunza.
 

Endelea kusoma: elimu

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri