Twaweza.org

Gharama za kutibu Malaria

Maduka kadhaa ya dawa jijini Dar es Salaam yanaendelea kuuza dawa ya kutibu malaria kwa bei isiyo sahihi kwa dozi za watoto na watu wazima.

Matokeo haya yalitolewa katika muhtasari ulioendeshwa na Shirika la Vijana la Kujitolea Tanzania (Youth Initiatives Tanzania, YITA) uitwao: Gharama ya kutibu malaria: Je, Serikali, wahisani, sekta binafsi na wananchi wanaweza kuhakikisha dawa za gharama nafuu? Matokeo hayo yanatokana na utafiti uliofanyika katika maduka ya dawa 58 yaliyopo katika wilaya zote tatu za jiji la Dar es Salaam. Wafanyakazi wa YITA walitembelea maduka haya na kununua dawa ya Artemether-lumefantrine (Alu), ambayo ni dawa inayopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutibu malaria.

Dawa ya Alu ilichaguliwa kufuatia mpango wa majaribio wa Dawa Nafuu za Malaria (AMFm). Mpango huu uliofadhiliwa na Mfuko wa Ulimwengu wa Kupambana na UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria ulianzishwa ukiwa pia na nia ya kuwezesha uagizaji bidhaa katika sekta binafsi na za umma kufanikiwa kununua dawa ya Alu yenye ruzuku. Tanzania ni miongoni mwa nchi saba za Afrika zilizoshirikishwa katika majaribio ya AMFm na kutoa matokeo ya kuwa bei ya dozi ya mtu mzima iwe TZS 1,000 na ile ya mtoto iwe TZS 500. Bei hii imehimizwa kupitia vituo vya televisheni na redio na hata matangazo yanayobandikwa hasa katika maeneo ya umma. Matangazo haya yalitolewa kupitia taarifa za ofisi ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuanzia Julai na Agosti 2011. Mabango na vipeperushi pia vilitumika kuhamasisha jamii vikionyesha bei ya Alu inayoelekezwa na Serikali.

Utafiti uliibua mambo yafuatayo:

  • Kati ya maduka ya dawa 55 yaliyouza dozi ya mtoto ya Alu, karibu yote yalidai TZS 1,000 au zaidi. Ni duka moja tu ndilo lililokuwa likiuza dawa hiyo kwa bei sahihi ya TZS 500 kwa dozi hiyo ya mtoto.
  • Kwa upande wa dozi ya watu wazima, ilibainika kuwa duka moja kati ya mawili (48%) yaliuza Alu kwa bei zaidi ya TZS1,000. Karibu robo (23%) ziliuza Alu kwa TZS2,000 au zaidi.
  • Vilevile, kulikuwa na tofauti katika wilaya moja hadi nyingine – wilaya tajiri zilikuwa uwezo mkubwa zaidi wa kuuza Alu kwa bei kubwa zaidi. Karibu nusu ya maduka ya dawa Kinondoni (47%) yaliuza Alu kwa TZS 2,000 au zaidi wakati katika wilaya ya Temeke, zaidi ya robo tatu (79%) ya maduka ya dawa yaliuza Alu kwa bei iliyopendekezwa ya TZS 1,000.

Endelea kusoma: afya

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri