Twaweza.org

Matarajio lukuki: Maoni ya wananchi kuhusu sekta ya gesi

Wananchi wengi hawana taarifa sahihi kuhusu gesi asilia iliyogundulika hivi karibuni nchini Tanzania.

Asilimia 53 wanafikiri kuwa gesi iliyogunduliwa pwani ya Tanzania tayari inavunwa na inazalisha mapato (makadirio yanaonesha kuwa hadi mwaka 2025 ndipo gesi itakapoanza kuvunwa). Pia, wananchi 6 kati ya 10 wanaamini kuwa Serikali na makampuni ya kigeni tayari yameshaanza kuingiza mapato kutokana na gesi hii (kitu hiki kitawezekana pale ambapo gesi itaanza kuvunwa kwa ajili ya matumizi).

Watanzania wanatarajia kwamba kila mwananchi atapata Sh. milioni 7.5 kutokana na gesi katika kipindi cha miaka kumi. Makadirio kaya yanapingana na hali halisi ya mapato ya gesi kwa kila mtu ambayo yanakadiriwa kuwa ni Sh milioni 2.5; hii ni theluthi moja tu ya matarajio ya wananchi. Pia, takriban wananchi 2 kati ya 10 (au 17%) wanafikiri wataajiriwa katika sekta hiyo. Hii ni ishara ya wananchi kuwa na imani kwamba ajira milioni nne zitajitokeza kutoka katika sekta hii ya gesi. Sekta ya gesi nchini Norway hutoa ajira kwa watu 240,000 tu.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza katika muhtasari wa utafiti wenye jina la Matarajio lukuki| Maoni ya wananchi kuhusu sekta ya gesi. Muhtasari huo unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika mara kwa mara kupitia simu za mkononi. Matokeo yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka awamu mbili za kupiga simu. Jumla ya washiriki 1,562 Tanzania Bara (Zanzibar haimo katika matokeo haya) walihojiwa kati ya mwezi Oktoba na Desemba 2013 na, hivi karibuni, washiriki 1,316 walihojiwa kati ya mwezi Aprili na Mei 2015.

Mbali na kupata ajira mpya na fedha nyingi, asilimia 51 wanatarajia gesi asilia italeta umeme wa uhakika (kwa sasa ni wananchi zaidi ya 10% tu waliounganishwa na gridi ya taifa). Asilimia 46 nao wanatarajia gesi ya kupikia itauzwa kwa bei nafuu.

Hata hivyo wananchi wana wasiwasi juu ya mgawanyo wa mapato ya gesi. Wengi wanahofia viongozi wa Serikali (33%) au matajiri (22%) watafaidika zaidi na mapato haya. Mwaka 2013, asilimia 31 ya wananchi walifikiri nchi nzima ingeweza kunufaika kwa usawa, lakini idadi hiyo imeshuka hadi asilimia 22 mwaka 2015.
 

Endelea kusoma:

Authors: Angela Ambroz

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri