Twaweza.org

Nyota njema huonekana asubuhi: Maoni ya wananchi kuhusu huduma za afya

Utafiti wa Sauti za Wananchi wa Twaweza unaonyesha maoni chanya kutoka kwa wananchi juu ya sekta ya afya nchini Tanzania. Kwa mfano, ni asilimia 18 wananchi wanaoripoti kuona upungufu wa madaktari katika vituo vya afya miezi mitatu iliyopita, ukilinganisha na asilimia 43 walioliona tatizo hili mwaka 2015. Vilevile, asilimia 73 walisema waliheshimiwa ipasavyo mwaka 2016, idadi hii ikiongezeka kutoka asilimia 42 mwaka 2015. Usafi kwenye vituo vya afya ulionekana kuboreshwa mwaka 2016. Waliolalamikia jambo hili walipungua kutoka watu 3 kati ya 10 mwaka 2015, hadi mtu 1 tu kati ya watu 10 mwaka huu. Vilevile, malalamiko yahusuyo kushindwa kumudu gharama za matibabu pia yalipungua: mwaka 2015, asilimia 34 ya wananchi walisema gharama zilikuwa kubwa mno au hawakuweza kulipa gharama hizo huku mwaka 2016, asilimia 19 ndio waliolalamikia gharama hizo. Hata hivyo, upungufu mkubwa wa dawa na vifaa vingine muhimu vya afya bado ni tatizo sugu: mwaka 2015, asilimia 53 walisema hivyo ukilinganisha na asilimia 59 mwaka 2016.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kupitia muhtasari wa utafiti wake wenye kichwa cha habari cha Nyota njema huonekana asubuhi? Maoni ya wananchi kuhusu huduma za afya zinazotolewa na serikali ya awamu ya tano. Muhtasari huo unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi. Matokeo yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,836 kutoka maeneo mbalimbali Tanzania Bara kati ya tarehe 2 na 17 Mei 2016 (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya).

Mwaka 2016, asilimia 61 ya Wananchi waliripoti kutibiwa katika vituo vya afya vya serikali. Hili lilikuwa ni ongezeko la mahudhurio ukilinganisha na asilimia 47 mwaka 2015. Kwa upande wa maduka ya dawa, wananchi waliotembelea maduka haya walipungua kutoka asilimia 19 mwaka 2015 hadi asilimia 13 mwaka 2016. Wale walioamua kutochukua hatua yoyote walipougua walipungua kutoka asilimia 8 mwaka 2015 hadi asilimia 2 mwaka 2016.

Asilimia 73 waliripoti kusubiri kwa muda usiozidi lisaa limoja kabla ya kumuona daktari. Wengi wao walikiri kupewa maelezo mazuri kuhusu maradhi yanayowasibu (asilimia 92) na kuandikiwa dawa stahiki (asilimia 81). Asilimia 70 walifanikiwa kupata angalau baadhi ya dawa walizozihitaji kutoka kwenye kituo hicho hicho cha afya.

Zifuatazo ni baadhi ya picha kwa ajili ya matumizi ya vyombo vya habari (bonyeza kulia juu ya picha ili kuweza kutumia katika ukurasa mwingine) pamoja na baadhi ya machapisho yaliyotolewa sambamba na uzinduzi huu.

    

Endelea kusoma:

Authors: John Mugo

pakua nyaraka

Tafsiri

unaweza pia kupenda...

 

Tafsiri