Twaweza.org

Mpya

Wanawake wa Mwanga Kusini, Kigoma wanakabiliwa na ubakwaji na ukatili

Wanawake wengi wa Kigoma wanaishi kwa hofu tangu mwaka 2016 kutokana na uhalifu unaojulikana kama Teleza. Wanawake, hususan wale wanaoishi bila wanaume katika nyumba zao, wako kwenye hatari ya kuvunjwa kwa nyumba zao na watu wasiojulikana kisha kubakwa au, wakijaribu kuwazuia, kufanyiwa ukatili na kujeruhiwa.

Simulizi binafsi za wanawake hawa zimewekwa hadharani na umoja wa asasi za kiraia (AZAKI) ikiwa ni pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Tamasha, Change Tanzania, Kituo cha Madai Mkakati, Jamii Forums, na Twaweza. Uhalifu huu almaarufu Teleza uliibuliwa wakati baadhi ya AZAKI hizi zikifanya kazi mkoani Kigoma.

Takwimu kamili juu ya kiwango cha matukio hayo bado hazijapatikana kutokana na changamoto za ukusanyaji wa takwimu kuhusu ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na utayari wa wanawake wengi kusita kutoa taarifa kutokana na hofu ya watu kuwanyanyapaa au wahalifu kulipiza kisasi. Hata hivyo, katika siku tatu za kuchunguza jambo hilo kwa kuwaendea wanawake wenyewe, AZAKI ziliweza kutambua na kuandika habari za matukio zaidi ya 45 yaliyoanza mwaka 2016 na kuendelea hadi mwaka huu.

Matukio haya ya ubakaji yanafanana kwa mambo kadhaa:

 • Wanaofanyiwa ukatili huu ni wanawake ambao wanaishi bila wanaume ndani ya nyumba zao (wake wenza, wajane, waliotalikiwa au kuachika, wasichana wadogo, wanawake wazee, na wanawake ambao waume zao wamesafiri)
 • Wabakaji huvua nguo na kujipaka oili chafu au mafuta mengine ili wasiweze kukamatika kirahisi. Hapa ndipo jina la Teleza lilipopatikana.
 • Wabakaji huwadhoofisha wanawake wenyewe pamoja na kuwazuia majirani zao au wanakaya wengine kwa kutumia dawa za kuwafanya wasinzie au kwa kuwafungia ndani ya vyumba au nyumba zao.
 • Wanaume hawa huwa na silaha, hasa visu, mapanga na viwembe ambavyo huvitumia kwa kujihami, kuwatishia na kuwazuia wanawake wasipige kelele. Hata hivyo wanawake wengi wanajitahidi kujihami na matokeo yake ni kwamba wanajeruhiwa kwa silaha hizo. Mara nyingi, wanaokaa kimya hurudiwa na kubakwa tena siku nyingine.

Mbali na madhara ya wazi ya kimwili na kisaikolojia, hali hii pia husababisha athari kubwa nyingine kama vile:

 • Vifo vya waathirika
 • Kuvunjika kwa ndoa/mahusiano - wanawake ambao wako katika mahusiano mara nyingine huachwa baada ya kuwa wahanga wa ukatili huo. Kinyume chake, wengine hulazimika kurudia waume zao licha ya ukatili au udhalilishaji wao.
 • Kudumaa kwa uchumi binafsi kutokana na wanawake kushindwa kufanya baadhi ya kazi mara tu baada ya kushambuliwa na mara nyingi hulazimika kuchukua mikopo au kuuza mali kulipia matibabu yao.
 • Hatari kubwa ya kuambukizwa VVU na magonjwa mengine ya ngono.
 • Hatari ya kupewa mimba zisizotarajiwa.
 • Wanawake wa maeneo haya kuishi kwa hofu juu ya usalama wao

Inaonekana kwamba wanajamii na viongozi katika eneo hilo hawajalipa uzito suala la wanawake hawa na ukatili unaofanywa dhidi yao. Waathirika wa mashambulizi haya ya kutisha wanafukuzwa, wanachekwa na kukejeliwa pamoja na kudhalilishwa na polisi (ambao mara nyingi ni wanaume). Hata wakati wanapowataja wahalifu na kutoa ushahidi, ama hakuna hatua inayochukuliwa ama wanaume hawa hukamatwa kwa muda mfupi na kisha kuachiwa. Jamii pia huwashutumu wanawake hawa kuwa ni makahaba, au kujenga dhana kwamba, kwa namna fulani, wanastahili kufanyiwa ukatili huo. Wakati waathirika wakihangaika kutafuta matibabu, huongezewa uchungu kwa kutakiwa kulipa shilingi elfu tano (TZS 5,000) kwa ajili ya fomu za PF3, elfu 30,000 kwa ajili ya kushonwa na gharama nyingine za matibabu, pamoja na kuulizwa maswali mengine ya kufedhehesha.

Kutokana na uhalifu huu wa kutisha, AZAKI zetu kwa pamoja tunataka:

 • Waziri wa Mambo ya Ndani kufanya ziara mahsusi katika wilaya ya Kigoma Ujiji ili kushughulikia swala la Teleza ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano na wanawake waathirika, viongozi wa eneo na polisi.
 • Wizara ya Mambo ya Ndani kutoa taarifa rasmi kwa umma kupitia vyombo vya habari kulaani mtindo wa Teleza na kuhakikisha kwamba hatua za haraka zinachukuliwa dhidi ya wote waliohusika.
 • Kuunda kikosi kazi maalumu kitakachojumuisha maafisa wa polisi, viongozi wa eneo na wawakilishi kutoka vikundi vya wanawake ili kuchunguza na kushughulikia suala hilo.
 • Kuanzisha mijadala wa wazi na waathirika pamoja na AZAKI zetu, na wawakilishi wa serikali kuu na serikali ya manispaa ili kubuni mbinu za utoaji elimu ya umma, kuongeza misaada ya kijamii kwa waathirika wa ukatili huu wa kutisha.
 • Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kushirikiana na mashirika ya msaada wa wanawake ili kuboresha uwezo wa dawati la jinsia la polisi liweze kutoa msaada wa kiutu kwa waathirika huko Kigoma-Ujiji na mahali pengine

Churchill Shakim, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamasha alisema "Simulizi hizi zinaweka wazi mateso ya wanadamu yaliyokutana na uzembe kwa upande wa mamlaka. Tumedhamiria kuwaunga mkono wanawake wa Mwanga Kusini waweze kupaza sauti zao na kudai kurejeshewa usalama wa kaya zao na jamii yao."

Wakilii Anna Henga, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, alisema "Wajibu wa kwanza wa serikali ni kuhakikisha usalama wa raia, hasa wale ambao hawawezi kujilinda wenyewe. Ubakaji unaoendelea huko Kigoma unapaswa kuchochea kuchukuliwa hatua sahihi na za haraka. "

Deus Valentine Rweyemamu, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Madai Mkakati, alisema "Ukosefu wa majibu kutoka kwa polisi na mamlaka nyingine unaongeza uchungu wa majeraha ya wanawake hawa. Tunahitaji kuimarisha utamaduni wa utawala wa sheria katika nchi kiasi kwamba hatutakusikia tena simulizi za za waathirika wasio na nguvu ambao hawapatiwi faraja wala msaada kutoka kwa wale wanaohusika na kuwalinda. "

Mshabaha Mshabaha, Mratibu wa Taifa wa ChangeTanzania, alisema "Wakati wanawake wanapoteseka, familia na jamii huteseka pia. Teleza inatoa changamoto ya wazi kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii huko Kigoma. Tunavisihi vyombo vya usalama nchini kushughulikia suala hili kwa uzito mkubwa sana. Raia yeyote hapaswi kujisikia hayuko salama na kuwa na hofu kwa muda mrefu hivyo.”

Maxence Melo, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums, alisema "Tuna wajibu na jukumu la kuongezea nguvu ya sauti za wale ambao hawana uwezo wa kufikia majukwaa na nafasi sawa na sisi. Huu ndio msingi wa kazi ya asasi za kiraia - kuhakikisha kuwa wasio na sauti, waliopuuzwa na wenye mahangaiko ya muda mrefu wanasikilizwa."

Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, alisema: "Simulizi hizi zinaelezea jamii ya Kigoma iliyo chini ya udhalimu. Lazima tuchukue hatua za haraka ili kupunguza matatizo haya ya wanawake. Na tunahitaji kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kuwa hakuna pembe nyingine za nchi hii ambazo wanawake huteseka kimya kimya namna hii. "

Wanachama wa Umoja huo ni Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, TAMASHA, Kituo cha Madai Mkakati, ChangeTanzania, JamiiForums na Twaweza.

 

Endelea kusoma: Citizen Agency

Kuhusu mtunzi

unaweza pia kupenda...