Twaweza.org

Mpya

Taarifa kuhusu Muswada wa Marekibisho ya Sheria Mbalimbali (Miscellaneous Amendments) No. 3 (2020)

Siku ya Alkhamis, Juni 4, Serikali ilichapisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Miscellaneous Amendments No.3 (2020), ikikusudia kurekebisha Sheria 13. Siku ya Ijumaa, Juni 5 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria iliwatangazia wadau kuwa wanakaribishwa kutoa maoni kwa siku tatu kuanzania Ijumaa Juni 5 mpaka Jumapili Juni 7 kabla ya hatua nyingine kuendelea. Muswada huu uliwasilishwa kwa hati ya dharula na hivyo kupelekea zoezi la kukusanya maoni ya wadau kufanyika kwa haraka hata siku za mapumziko mwisho wa wiki.

Kipekee kabisa, marekebisho haya yanayopendekezwa yanagusa kiini cha jamii yetu, hususan dhana ya utawala wa sheria.

Sisi, asasi huru za kiraia tunaotetea na kuenzi misingi muhimu ya uhuru na demokrasia, tungependa kuigutusha jamii nzima kuhusu athari zinazoweza kutokea iwapo Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali No. 3 (2020) utapita bila kuboreshwa.

Kiholela kabisa, marekebisho mengi yanayopendekezwa yanakiuka maana na dhamira ya Katiba yetu. Mapendekezo haya yanahatarisha misingi muhimu kabisa ya Katiba kama vile usawa mbele ya sheria (Ibara ya 13), Katiba kuwa ndio sheria kuu (Ibara ya 26), na mgawanyo wa madaraka baina ya mihimili ya dola (Ibara ya 4). 

Ibara ya 13 – Usawa mbele ya sheria uko hatarini!

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatamka kwamba:

‘13(1) Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria.’

Marekebisho yanayopendekezwa kwenye Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama (Sura ya 237) yanaweka kinga dhidi ya kushtakiwa kwa watendaji wote katika mfumo wa mahakama kwa matendo waliyofanya kwa “nia njema” wakati wa ajira zao.

Marekebisho yanayopendekezwa kwenye Sheria ya Maboresho ya Sheria Kuhusu Ajali Mbaya na Msharti Mengineyo (Sura ya 310) na Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi, (Sura ya 3) pia yanasema mashtaka yote dhidi ya Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika, Naibu Spika au Jaji Mkuu hayawezi kuletwa moja kwa moja dhidi yao bali mashtaka hayo yanatakiwa kuletwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Kwa kuwalinda watu wenye nyadhifa hizo dhidi ya kushtakiwa mahakamani, marekebisho haya ya sheria yanadhoofisha uwajibikaji nchini. Uzoefu toka nchi nyingine duniani umeonesha kuwa, mara nyingi, wahusika wanapowajibishwa wao wenyewe moja kwa moja huwa wanakuwa makini katika utendaji wao kuepusha makosa yasiyokuwa ya lazima. Dhana ya usawa mbele ya sheria kama ilivyobainishwa kwenye Katiba yetu inataka kwamba, kila mmoja wetu, bila kujali hadhi au nafasi yake, anatakiwa kuwajibishwa mbele ya sheria. Marekebisho haya yanaweka upendeleo kwa kuzingatia hadhi na nyadhifa za wahusika pindi wanapokiuka Katiba na Sheria tofauti na dhana ya usawa wa watu wote mbele ya sheria inavyoelekeza. Vile vile, hakuna mantiki ya kuwaongezea kinga kwa sababu Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Sheria ya Mahakama tayari zinatoa kinga za kutosha za kuwawezesha watendaji hawa kutekeleza majukumu yao.

Ibara ya 26 – Shambulizi dhidi ya hadhi ya Katiba kama sheria kuu!

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatamka ifuatavyo:

 ‘26(2) Kila  mtu  ana  haki,  kwa  kufuata  utaratibu  uliowekwa  na  sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za nchi.’

Mapendekezo ya marekebisho Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi (Sura ya 3) yanaelekeza kwamba wanaoweza kufungua kesi za kikatiba ni wale tu ambao wameathiriwa moja kwa moja na swala husika. Mapendekezo hayo yamekwenda mbali zaidi kwa kuelekeza kwamba Ibara ya 30 (Kifungu cha 3) ya Katiba itumike kufafanua Ibara ya 26 (Kifungu cha 2) ya Katiba.

Mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Maboresho ya Sheria Kuhusu Ajali Mbaya na Masharti Mengineyo (Sura ya 310) na Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi (Sura ya 3)

yanawapa watu mahsusi kinga dhidi ya kushtakiwa wanapokiuka Katiba katika mazingira mahsusi.

Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamuwezesha kila Mtanzania kulinda na kuheshimu Katiba kwa njia mbali mbali ikiwemo kutumia utaratibu wa Mahakama. Kuondoa haki ya raia kufungua mashtaka mpaka tu pale ambapo wanakuwa wameathiriwa moja kwa moja inaondoa haki ya kisheria ya raia na taasisi kufungua mashtaka kwa maslahi ya umma. Kwa kuongezea, kuwapa baadhi ya watu kinga dhidi ya kushtakiwa kwa makosa ya Kikatiba inawanyima raia na taasisi haki na uwezo wa kulinda Katiba yetu. Muhimu zaidi ni namna ambavyo marekebisho haya yatazipa sheria na taratibu za kuunda sheria kuwa na hadhi na mamlaka ya juu zaidi ya Katiba kinyume inavyoeleweka kuwa Katiba ya nchi ndio sheria mama na ya juu kuliko sheria zote kwenye taifa lolote lile.

Ibara ya 4 – Mgawanyo wa Madaraka Unadhoofishwa!

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatamka kwamba:

‘4(1) Shughuli zote za Mamlaka ya Nchi katika Jamhuri ya  Muungano  zitatekelezwa  na  kudhibitiwa  na  vyombo  viwili  vyenye  mamlaka  ya  utendaji,  vyombo  viwili  vyenye  mamlaka  ya   kutekeleza   utoaji   haki,   na   pia   vyombo   viwili   vyenye  mamlaka   ya   kutunga   sheria   na   kusimamia  utekelezaji  wa  shughuli za umma.’

Mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Maboresho ya Sheria Kuhusu Ajali Mbaya na Masharti Mengineyo (Sura ya 310) na Sheria ya Utekelezaji wa Haki na Wajibu wa Msingi (Sura ya 3) yanatamka kwamba mashtaka yote dhidi ya Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Spika, Naibu Spika au Jaji Mkuu hayawezi kuletwa dhidi yao moja kwa moja bali kwa kumshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa niaba yao.

Mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Uendeshaji Bunge (Sura ya 115) yanampa Rais mamlaka makubwa zaidi katika uendeshaji wa shughuli za Bunge – hususan mamlaka ya kuidhinisha uundwaji wa idara (departments), vitengo (units) na sehemu (sections) mbalimbali za Tume ya Huduma za Bunge.

Dhana ya mgawanyo wa madaraka ni msingi muhimu sana kwa Jamhuri na demokrasia yetu changa. Dola yetu ya Jamhuri ya Muungano ina mihimili mitatu ambayo ni Serikali (the Executive), Bunge (the Legislative) na Mahakama (the Judiciary). Kila mhimili ni huru na una jukumu la kuwa mlinzi kwa mihimili mingine kwa maslahi ya umma. Kwa mfano, Mahakama ina jukumu la kuhakikisha sisi sote tunafuata sheria halali za nchi. Marekebisho haya yanamfanya Mwanasheria Mkuu, ambaye ni sehemu ya Mhimili wa Serikali (the executive), kuwajibika kwa makosa ya kisheria yanayofanywa na viongozi wa juu kwenye mihimili yote mitatu ya Dola. Hii inafifisha mipaka ya uwajibikaji katika mihimili hii mitatu na pia inaondoa dhana muhimu ya mgawanyo wa madaraka na uwajibikaji.

Pia, kwa kumpa Rais mamlaka kwenye shughuli za kawaida za Bunge, marekebisho haya yanadhoofisha ama kuondoa kabisa mamlaka ya Bunge kuiwajibisha Serikali. Ni muhimu kuzingatia kuwa marekebisho yote yanayoathiri mamlaka na uhuru wa Bunge yanakinzana moja kwa moja na Ibara za 62 na 63 za Katiba ambazo zinabainisha majukumu ya Rais kwa Bunge na kwamba Bunge ni mhimili wa juu kabisa kwenye Jamhuri yetu.

Kwa maelezo haya, ni dhahiri kwamba mapendekezo ya marekebisho ya sheria mbalimbali  (Miscellaneous Amendments No. 3 of 2020) ni hatari sana kwa ustawi wa Jamhuri yetu ya Muungano. Tunawahimiza watunga sheria, vyombo vya habari, asasi za kiraia na wananchi wote kwa ujumla kuungana kupinga marekebisho haya hatarishi. Kwa kufanya hivyo, tutatimiza jukumu letu adhimu la kuilinda na kuiheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia kuendelea kujenga taifa letu kwa misingi ya demokrasia na utawala wa sheria.

Unga mkono waraka wa kupinga marekebisho haya kwa kuweka saini yako hapa

Fuatalia mdahalo:  #DemokrasiaYetu #Muswada2020 na hapa

Imetolewa na: Centre for Strategic LitigationJamiiForums, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (Legal and Human Rights Centre)Media Council of TanzaniaTanzania Human Rights DefendersTwaweza

Kwa taarifa zaidi:

The full joint submission

The written Laws (Miscellaneous Amendments) (no.3) Act, 2020

Interpretation of Laws Act

The National Assembly (Administration) Act

Basic Duties and Enforcement Act

The Presidential Affairs Act

Constitutional Excerpts Relevant to the Miscellaneous Amendments No. 3 Act, 2020

The Constitution of The united Republic of Tanzania

Endelea kusoma: analysis

Kuhusu mtunzi

unaweza pia kupenda...