Twaweza.org

Mpya

Nusu nusu? Maoni ya wananchi kuhusu upatikanaji wa maji safi

Asilimia 36 ya Watanzania wanapata huduma ya maji ya bomba. Hata hivyo, wengine wengi hutegemea maji ya visima (asilimia 35) au maji ya kwenye madimbwi (asilimia 18), ambayo kwa ujumla siyo safi na salama. Katika suala la upatikanaji wa maji, tofauti kati ya wakazi wa mijini na vijijini ni kubwa: asilimia 51 ya wakazi wa mijini wanapata maji ya bomba nyumbani kwao, ikilinganishwa na asilimia 11 tu ya wananchi wa vijijini. Licha ya kuanzishwa kwa Mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), na kumalizika kwa kipindi cha Malengo ya Maendeleo ya Milenia (MDGs), upatikanaji wa maji haujabadilika katika kipindi cha mwaka jana. Kwa ujumla, ni asilimia 41 tu ya wakazi wa vijijini wanaopata maji kutoka chanzo cha maji kilichoboreshwa ukilinganisha na asilimia 69 ya wananchi wa maeneo ya mijini.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye muhutasari wa utafiti wenye jina la Nusu nusu? Maoni ya wananchi kuhusu upatikanaji wa maji safi. Muhutasari huu umetokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika mara kwa mara kwa njia ya simu za mikononi. Matokeo yametokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,852 wa Tanzania Bara kati ya tarehe 9 Septemba na 26 Septemba 2015 (Zanzibar haikuhusishwa kwenye matokeo haya).

Takribani nusu ya wananchi wote (asilimia 44) hutumia zaidi ya dakika 30 kufuata maji kwa ajili ya mahitaji yao, wakati mwongozo wa serikali unapendekeza kuwa wananchi hawapaswi kutumia zaidi ya nusu saa kufuata maji kwa ajili ya matumizi ya kila siku. Katika maeneo yote ya mijini na vijijini, mwananchi mmoja kati ya watatu wametaja ukosefu wa vyanzo vya maji kama changamoto yao kubwa.

Kwa ujumla, wananchi wanakumbana na masuala kadhaa kwenye kupata maji, huku kukiwa na tofauti kubwa ya upatikanaji wa maji ndani ya jamii za vijijini na mijini. Kwa wakazi wa vijijini, changamoto yao kubwa ni umbali wa vyanzo vya maji (asilimia 47) na uchafu wa maji (asilimia 40). Kwa upande wa mijini, mgao wa maji (asilimia 43) na gharama kubwa za maji (asilimia 40) ndivyo vinavyowatatiza zaidi.

Asilimia 57 waliripoti kutumia njia mojawapo ya kutibu maji yao ili yawe salama. Wengi zaidi walisema walichemsha maji yao (asilimia 85). Idadi kubwa nao waliripoti kuchuja maji (asilimia 69) au kuyaacha yatuwame uchafu ubaki chini (asilimia 38). Hata hivyo, njia hizi kwa viwango vya kimataifa, hazikubaliki kama njia za kuyafanya maji yawe safi na salama.
 

Endelea kusoma:

unaweza pia kupenda...