Twaweza.org

Mpya

Fedha zinamiminika, maji kiduchu

Bajeti kwa ajili ya kuboresha huduma ya sekta ya maji imeongezeka karibu mara tano kati ya mwaka 1999/2000 na mwaka 2011/2012, lakini hakujawa na ongezeko la tarakimu wala ubora wa upatikanaji wa huduma ya maji safi katika kipindi hicho. Kinyume chake, kati ya mwaka 1990 na 2011, upatikanaji wa huduma ya maji ulishuka kutoka 55% hadi 53%.

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye muhtasari wa utafiti wenye jina la “Fedha zinamiminika, Maji kiduchu. Changamoto za upatikanaji wa maji safi nchini Tanzania’’. Muhtasari umetokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, utafiti wa kaya wenye uwakilishi wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu ya mkononi Tanzania bara.

Kati ya mwaka 1995 na 2005, Tanzania ilipokea misaada kwenye sekta ya maji inayolingana na dola za Kimarekani 57 kwa kila anayenufaika bado upatikanaji wa huduma ya maji ulishuka kwa 1%. Ikilinganishwa na nchi nyingine, Uganda ilipokea dola 16 kwa kila anayenufaika katika kipindi hicho hicho na walifanikiwa kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwa 25%, wakati Kenya ilipokea dola 17 kwa kila anayenufaika na walipata ongezeko la upatikanaji wa maji kwa 20%.

Kutokana na kushuka kwa upatikanaji wa maji safi licha ya uwekezaji mkubwa, kufanikisha malengo makubwa ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ya kufikia 75% ya Watanzania wanaopata maji safi na salama itahitaji mabadiliko makubwa kiutendaji. Kuongeza fedha kwa ajili ya sekta ya maji bila kufanya mapitio ya kina kujua sababu za kushindwa kutoa huduma siku za nyuma, kunaweza kusababisha makosa ya zamani kujirudia.

Karibu Mtanzania mmoja kati ya watatu (30%) anasema kuwa maji ni moja kati ya matatizo matatu makubwa yanayoikabili nchi yetu. Pengine haishangazi kutokana na ukweli kuwa hakuna maboresho ya upatikanaji wa maji kwa kipindi kirefu. Maji yamewekwa nafasi ya juu pamoja na afya kama changamoto ya msingi kwa Watanzania.

Changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama imeendelea kuwepo kwa watu wengi. Karibu Watanzania wote (89%) huchota maji kutoka vyanzo vya umma, hii ina maana kuwa ni mtu mmoja tu kati ya kumi (11%) ndiye mwenye bomba la maji nyumbani au maji yanaletwa nyumbani. Lengo rasmi la Serikali ni kuona watu wanatumia si zaidi dakika 30 tu (safari ya kwenda na kurudi) kuchota maji, lakini wastani wa muda halisi wanaotumia ni karibu saa moja (dakika 57).

Sauti za Wananchi pia iliuliza ni nani mwenye jukumu la kuchota maji kwenye kaya: katika kaya tatu kati ya nne, mwenye jukumu hilo ni mwanamke mkuu wa kaya ambaye ni lazima ahakikishe kuwa kaya ina maji kwa ajili ya mahitaji ya kila siku.

Marekebisho kidogo yamefanyika katika maandishi hayo hapo juu, muhtasari na taarifa kwa vyombo vya habari kuhusiana na takwimu za misaada iliyopokelewa kwa nchi za Kenya, Tanzania na Uganda. Hapo awali, takwimu zilisema ‘msaada kwa kila mtu’ wakati ambapo zilipaswa kumaanisha ‘msaada kwa kila anayenufaika’.

Endelea kusoma:

unaweza pia kupenda...