Twaweza.org

Mpya

Tamko kuhusu Marekebisho yanayopendekezwa kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa

Hivi karibuni, kumekuwa na mijadala kuhusiana na marekebisho yanayopendekezwa kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa (2002). Sisi kama taasisi huru ya kiraia ambayo inalinda haki/kanuni za kidemokrasia, tungependa kutoa maoni na kupaza sauti yetu kwenye mjadala unaoendelea tukiwa na lengo la kutafuta njia bora ya kusonga mbele, ambayo italinda demokrasia yetu changa huku ikipatikana njia sahihi ya kusimamia usajili wa vyama vya siasa.

Kwanza, uteuzi wa Msajili unaofanywa na Rais, ambao hapo awali ulipigiwa kelele, una maana kwamba, kiutendaji, ni vigumu kwa Msajili kutofungamana na upande wowote. Hivyo, kwa kumwongezea Msajili mamlaka zaidi ya kuingilia masuala ya ndani ya chama inaendelea kuminya usawa.

Ili kufafanua kwa mapana na marefu kuhusu marekebisho haya, tumetumia mfano wa mashindano ya mpira wa miguu. Kuna timu nyingi zinazoshindana (vyama) ambazo zote zinataka kupata ushindi. Kazi ya refa ni kuhakikisha kuwa timu zote zinashindana kwa haki na zinashinda kutokana na uwezo walionao. Marekebisho yanayopendekezwa kwenye Sheria ya Vyama vya Siasa yatasababisha mashindano yasiwe na usawa kwa sababu zifuatazo:

1. Refa ameajiriwa na moja ya timu inayoshiriki mashindano. Hivyo inakuwa vigumu kwa refa kutenda haki katika kipindi chote cha mchezo – mshahara wake unalipwa na moja ya timu na timu hiyo hiyo inaweza kumwondoa madarakani kama haijaridhishwa na utendaji wake.

Msajili anateuliwa na anaweza kuondolewa na Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa chama tawala.

2. Refa huyu ndiye anayefuatilia namna timu zote zinavyochagua wachezaji wa kucheza. Hata refa ambaye hafungamani na upande wowote hapaswi kuwa na mamlaka ya kuamkua wachezaji gani wacheze.

Marekebisho kwenye Kifungu cha 4 yanampa Msajili mamlaka ya kufuatilia michakato ya chaguzi na teuzi za ndani za chama.

3. Refa huyu ndiye anayehakikisha kuwa timu zote zinatumia fedha zake vizuri. Hili tena siyo jukumu ambalo tungetarajia refa alifanye lakini ni ukweli ulio wazi kuwa hawezi kufahamu kuhusu hali ya kiuchumi ya timu zingine wakati ana timu anayoipenda zaidi. Hii inaipa timu hiyo faida ya bure.

Marekebisho ya Kifungu cha 4 yanampa Msajili mamlaka ya kufuatilia mapato na matumizi ya vyama vya siasa na uwajibikaji wa rasilimali za chama.

4. Refa anaruhusiwa kudai taarifa YOYOTE kutoka kwenye timu yoyote. Hii inaipa faida ya bure timu iliyomwajiri.

Kifungu cha 5B kinamruhusu Msajili kudai taarifa yoyote kutoka kwenye vyama, na adhabu pia imewekwa; faini, kifungo na kufutiwa usajili.

5. Refa huyo anaweza akasitisha ruzuku kwa timu yoyote anayochagua. Kama kuna fungu la ruzuku linalotolewa kwa timu zilizofuzu kushiriki mashindano, refa hapaswi kupewa mamlaka ya kusitisha ruzuku hizo kiurahisi. 

Marekebisho ya kifungu cha 18 yanampa Msajili mamlaka ya kusitisha ruzuku kwa chama cha siasa kwa utashi wake kwamba chama hicho hakiwezi kusimamia ruzuku hiyo inavyopaswa.

6. Refa ana uwezo wa kuwazuia kabisa wachezaji wa timu yoyote kiasi hata cha kutoruhusiwa hata kuwa washabiki na kuangalia mchezo wakati ukichezwa uwanjani katika kipindi cha kusimamishwa.

Kifungu kipya cha 21E kinamruhusu Msajili kumsimamisha mwanachama yeyote wa chama cha siasa kwa kukiuka sheria hii. Usimamishwaji wa wanachama ni suala la ndani la chama. Adhabu yake inawazuia wanachama wa vyama hivi hata kupiga kura wakati wa chaguzi katika kipindi hicho ambacho wamesimamishwa.

Kwa kuongezea, yapo mambo kadhaa ambayo yamejitokeza kwenye marekebisho hayo:

Uhuru wa kujieleza

  • Vyama haviruhusiwi kufanya kazi kama vikundi vya uhamasishaji na kupigia debe masuala yenye maslahi kwa umma kwa lengo la kuwashawishi wananchi au serikali. Hii ni kazi ya msingi ya vyama vya siasa hivyo kifungu hicho kinavinyima vyama vya siasa kufanya kazi zake za msingi.
  • Faini pia zimewekwa kwa vyama vitakavyotoa kauli yoyote ambayo inaonekana si ya kweli. Siasa ni mahali ambapo ukweli huhojiwa, wanasiasa hutoa tafsiri tofauti tofauti, mawazo na sera zao, na wananchi hupata fursa ya kuchagua yule wanayempenda zaidi.

Kushirikiana na Kuungana

  • Vyama vinaruhusiwa tu kuungana ndani ya siku 21 kabla ya kupendekezwa kwa wagombea wa uchaguzi mkuu. Hiki ni kipindi kifupi sana kwa wao kuweza kufanya kampeni vizuri.
  • Kwa kuongezea, marekebisho yanapendekeza kuwa Waziri mwenye dhamana anaweza kutengeneza kanuni zitakazosimamia ushirikiano wa vyama. Hii inampa waziri, ambaye ni mwanachama wa chama tawala, mamlaka ya kuamua namna gani vyama vya siasa vitakavyoshirikiana na kufanya kazi pamoja.

Kusimamishwa

Wazo la kusimamisha vyama vya siasa kwa kipindi fulani limeongezwa kwenye marekebisho. Hata hivyo hakuna maelezo kuhusu sababu ambazo zitasababisha kusimamishwa huko, muda ambao vyama vimepewa kumjibu Msajili kuhusu mashaka aliyonayo kabla hajaamua kusimamisha chama au kinga yoyote dhidi ya usimamishaji wa vyama usio na msingi.

Kujenga uwezo

  • Chini ya kifungu kipya kinachopendekezwa, mashirika yanatakiwa kupata kibali kutoka kwa Msajili kabla ya kutoa elimu ya kujenga uwezo au elimu ya uraia kwa vyama vya siasa. Hakuna haja ya Msajili kuwa na mamlaka hii. Demokrasia ya Tanzania ni changa na inahitaji msaada kutoka sehemu mbalimbali.

Makundi maalumu

Katika Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa hakuna vifungu vinavyohakikisha ushiriki wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Sheria haijayahakikishia makundi haya muhimu nafasi ya kusikika na kujumuishwa kwa sauti zao katika kufanya maamuzi ndani ya vyama.

Tunaiomba serikali itoe muda wa kutosha kwa ajili ya kupitia marekebisho yaliyopendekezwa kwa kina, uwazi na ujumuishi ili kuhakikisha kuwa yanalinda na kudumisha maadili/haki za kidemokrasia hapa nchini Tanzania. 

Soma zaidi:

Tamko kuhusu Marekebisho yanayopendekezwa

Statement on Proposed Amendments

Five essential changes

Mabadiliko matano muhimu

The full joint submission

Why you should care about the amendments to the Political Parties Act?

Kwa nini tunajali kuhusu marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa?

Kwako Mbunge mzalendo - barua kwa Mbunge 

Tamko hili limewasilishwa na Legal and Human Rights CentreTanganyika Law Society, Centre for Strategic Litigation, the Media Council of Tanzania, Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar and Twaweza

Endelea kusoma: accountability

Kuhusu mtunzi

unaweza pia kupenda...