Tamko kutoka Wenyeviti Wenza wa Kamati ya Utendaji ya Open Government Partnership (OGP) kuhusu Ukraine.
“Tunalaani vikali shambulio dhidi ya nchi ya Ukraine, ambayo ni nchi mwanachama wa Open Government Partnership (OGP) tangu mwaka 2011, pasipo wao kufanya uchokozi wowote dhidi ya Urusi. Tunatoa wito kwa jumuia zote zinazoheshimu misingi ya serikali ya uwazi kukemea shambulio hili kwa haraka na nguvu zote.
Kama mwanachama wa OGP, Ukraine imekuwa ikipiga hatua madhubuti kuimarisha demokrasia yao, na kusukuma mbele maendeleo ya nchi yao. Yamekuwepo mageuzi ya kupigiwa mfano katika nyanja mbalimbali kama vile uuzaji na ununuaji wa mali za umma. Kazi hii imekuwa ikifanywa kwa ubia mkubwa kati ya serikali, asasi za kiraia na vyombo vya habari. Ukraine imekuwa nchi ya kupigiwa mfano na wengi wanaotaka kufuata mwenendo wa jitihada za nchi hiyo.
Wanamageuzi wa ndani na nje ya serikali ya Ukraine wameonesha ujasiri mkubwa na ustahimilivu wa hali ya juu hasa pale ambapo pamekuwepo na vitisho vingi kutoka nje ya nchi. Tunasimama pamoja na watu wa Ukraine wakati huu mgumu wanapokabiliana na uvamizi wa nje unaolenga kudhoofisha matumaini yao, kubadilisha uongozi uliopo madarakani na unaokumbatia mageuzi na taasisi za kidemokrasia na kuharibu kazi yote nzuri ambayo imekuwa ikiifanya Ukraine kuwa nchi ya kidemokrasia inayowahudumia vyema wananchi wake.
Kama Jumuiya, yatupasa kufanya kila liwezekanalo kuisaidia na kuilinda Ukraine.”
Imetiwa saini na Wenyeviti Wenza wa Open Government Partnership:
Serikali ya Italia
Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji, Twaweza East Africa
Serikali ya Estonia
Anabel Cruz, Mkurugenzi wa ICD Uruguay